Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi yajipanga Sikukuu ya Pasaka

3e970a969e6c4cda2552eff2ba9c3a8d Leo ni maadhimisho ya Ibada ya Ijumaa Kuu

Fri, 15 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la polisi limejiimarisha kushirikiana na viongozi wa dini na kamati za ulinzi katika nyumba za ibada kuhakikisha ibada na sherehe za Pasaka zinafanywa katika mazingira ya amani, utulivu na usalama.

Aidha, limewaomba viongozi wa dini, waumini na Watanzania kwa ujumla kutoa ushirikiano kuelimishana, kukemea maovu ndani ya familia, jamii yakiwamo ya unyanyasaji na ukatili unaosababisha mauaji, kujeruhi, kutelekeza familia, kubaka na kulawiti.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana Dodoma na Msemaji wa jeshi hilo, David Misime, imewatakia Watanzania wote Pasaka njema na kuwataka kuisherehekea kwa amani, upendo wa utulivu.

“Jeshi la Polisi linachoomba kwa viongozi wa dini, wanajamii na waumini ni ushirikiano, tuelimishane tukemee maovu kama baadhi ya waendesha vyombo vya moto kutofuata sheria za usalama barabarani na kusababisha vifo, ulemavu na uharibifu wa mali,” alisema Misime.

Alisema katika sherehe hizo za Pasaka, ulinzi umeimarishwa ili kuhakikisha zinafanywa kwa amani na utulivu na kuwaomba wananchi kuendelea kulipa jeshi hilo ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao.

“Tunawashukuru kwa ushirikiano wa wananchi umewezesha kupata mafanikio ya majukumu yetu katika doria, misako na operesheni mbalimbali na makamanda wa mikoa na kipolisi wamekuwa wakitoa taarifa za mafanikio hayo na hali hiyo imeifanya nchi kuendelea kuwa shwari,” alisema Misime.

Alisema katika wiki hii ya mfungo wa Kwaresma kuelekea Pasaka, kumekuwepo na ibada mbalimbali mchana na usiku katika nyumba za ibada hivyo katika kuhakikisha usalama unaendelea wameimarisha ushirikiano na viongozi wa dini.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema walikubaliana kufanya operesheni ndani ya kanda namba mbili inayohusisha mikoa ya Kipolisi ya Ilala, Temeke, Kinondoni, Pwani na Rufiji ili kukabiliana na uhalifu.

Alisema makubaliano hayo yalifanywa kwa lengo la kupambana na makosa makubwa ya uhalifu kama unyang’anyi wa kutumia silaha, wizi wa magari, pikipiki, bajaji, dawa za kulevya, uvunjaji na kuiba na wizi wa mifugo.

Mafanikio ya operesheni hiyo ni kukamatwa kwa watuhumiwa 632 waliokamatwa kati ya Machi 21, mwaka huu hadi Aprili 8, mwaka huu ambao baadhi walikutwa na silaha zikiwamo bunduki tano, risasi 53, magari ya wizi tisa, pikipiki 65 na mitambo ya kutengenezea pombe haramu ya gongo.

Aidha, katika operesheni hiyo walikamata dawa za kulevya heroin kete 88 na gramu 250, bangi gunia 31 na mirungi, jino moja la tembo na vifaa mbalimbali vya kielektroniki vilivyotokana na matukio ya kuvunja nyumba.

Pia waliwakamata madereva kwa makosa mbalimbali ya barabarani yakiwamo mwendokasi, kuyapita magari mengine na kuhatarisha maisha. Pia walikamatwa raia 45 wa Ethiopia na Somalia.

Kamanda Muliro alisema operesheni hiyo imesaidia kupunguza uhalifu na wamekubaliana itaendelea bila kujali mipaka kwa lengo la kupambana na wahalifu katika maeneo hayo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live