Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi yaanza uchunguzi tukio la mtoto kuuawa kwenye mahafali

A9605F97 702E 4E6A .jpeg Polisi yaanza uchunguzi tukio la mtoto kuuawa kwenye mahafali

Sun, 6 Nov 2022 Chanzo: Mwananchi

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limeanza uchunguzi wa tukio la mauaji ya mtoto, Ibrahim Shakiru (16) likidai aliuawa kwa kipigo kutoka kwa wananchi waliomkuta na panga kwenye mahafali ya kidato cha nne ya Sekondari ya Kirumba, iliyopo wilayani Ilemela mkoani hapa.

Kwa mujibu wa bibi wa Ibrahim, Nyamisi Masinye (73) mjukuu wake alishushiwa kipigo hicho Jumapili Oktoba 22, mwaka huu na watu anaowataja kuwa ni askari wa polisi jamii na walimu waliohudhuria kwenye mahafali shuleni hapo.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi mkoani humo limedai kijana huyo ambaye alifariki katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando akipatiwa matibabu, alishambuliwa na wananchi wenye hasira baada ya kumkuta na panga kwenye koti alilokuwa amevaa katika mahafali hayo.

Kaimu Kamanda wa Polisi (RPC) Mkoa wa Mwanza, Mairi Makori alisema jeshi hilo limefungua jalada la uchunguzi, kuwabaini watu waliohusika kumshambulia na kusababisha kifo cha mtoto huyo.

Alisema uchunguzi wa awali umeonyesha katika purukushani ya kumnyang’anya panga kijana huyo, mlinzi wa shule hiyo, Benedict Mwita na mwalimu, Mtaki Leonard walikatwa na panga hilo mikononi.

“Taarifa ya awali ni kwamba tumebaini yule kijana alikuwa na tabia za kihalifu, unaendaje kwenye sherehe ukiwa na panga. Lakini hiyo haihalalishi kumtoa mtu uhai, ndiyo maana tumeanza uchunguzi tukibaini waliohusika tutawakamata,” alisema Makori.

Makori, ambaye ni Mkuu wa Operesheni za Polisi mkoani humo aliitaka familia ya mtoto huyo, kufika ofisini kwake kwa ajili ya kupatiwa taarifa ya uchunguzi. Wakati Polisi ikitoa taarifa hiyo, mwili wa Ibrahim ulizikwa Jumatatu Oktoba 31, 2022 katika makaburi ya Kirumba wilayani Ilemela mkoani Mwanza, huku Imamu wa Msikiti wa Kabuhoro uliposwaliwa mwili wa mtoto huyo kabla ya mazishi, Rashid Juma aliomba waliohusika kwenye mauaji hayo wachukuliwe hatua.

“Jukumu la kutoa uhai wa mwanadamu ni la Mungu, tunashindwa kuelewa kwa nini watu wanaamua kujichukulia sheria mkononi na kuondoa uhai wa wenzao. “Tunaomba mamlaka husika zichukue hatua kali dhidi ya wahusika, itampendeza hata Mungu,” alisema Juma.

Kauli ya familia Bibi wa mtoto huyo, Nyamisi Masinye aliieleza Mwananchi kuwa uamuzi wa kutozika mwili huo, ulibatilishwa baada ya kuona hakuna majibu wala hatua zinazochukuliwa dhidi ya watu waliohusika kumshambulia. Nyamisi alisema hadi kufikia uamuzi wa kuzika mwili wa mpendwa wao, familia ilikuwa haijapewa majibu ya uchunguzi, huku akisema anaamini wahusika watachukuliwa hatua na kuahidi kwenda kwa RPC kuchukua taarifa hiyo.

“Suala la mjukuu wangu namuachia Mungu, sasa hivi sina mtu wa kunihudumia kwa sababu ndiyo alikuwa tegemeo langu.

“Alihakikisha ninaishi bila shaka, lakini sasa sina mtu wa kunisaidia mahitaji, nawaomba wasamaria wema watusaidie,” alisema Nyamisi. Kwa upande wa ndugu wa Ibrahim, Fadhiri Kachwamba alisema anaamini Jeshi la Polisi halitakaa kimya kuhusu mauaji ya ndugu yao. Alisema familia ina maswali mengi kuhusu uchunguzi wa kifo cha ndugu yao unavyoendelea na ambavyo imechukua muda angalau kuambiwa kuwa kuna majibu. “Mimi sina uelewa wa sheria, tumekuwa tukizungushwa tu kituoni hatuoni juhudi zozote za polisi kuwatia mbaroni waliotekeleza mauaji ya ndugu yetu, ndiyo maana tumeamua tuzike ili mwili usiharibike kisha hatua nyingine ziendelee. “Tunaiomba Serikali ikiwezekana iunde timu ichunguze suala hili kwa sababu hatuna imani na polisi, kwani miongoni mwa wanaotajwa kuhusika kumshushia kipigo ndugu yetu ni polisi jamii wawili na walimu, sidhani kama wanaweza kujichunguza,” alisema Kachwamba.

Chanzo: Mwananchi