Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi wawili, wafanyabiashara mbaroni tuhuma za utoroshaji madini

E88b2536d63e2e1b4f00952eafd4bbf8 Polisi wawili, wafanyabiashara mbaroni tuhuma za utoroshaji madini

Fri, 11 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ASKARI Polisi wawili, wafanyabiashara wakubwa wa madini wawili na mchimbaji mdogo wa madini mmoja, wamefunguliwa mashtaka kwa tuhuma za kutorosha madini katika tukio lililotokea Novemba 25 mwaka huu wilayani Chunya mkoani Mbeya.

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari hii leo.

Mganga aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni askari polisi Koplo Hassan Njujilo mwenye namba E.8970 na askari polisi Daniel Mrema mwenye namba G.7757 wote wa Wilaya ya Chunya.

Watuhumiwa wengine ni wafanyabiashara ya madini akiwemo Sabra Ally na Malof Nassor na mchimbaji mdogo wa madini Hamdun Mtafuni wote wa kutoka Wilaya ya Chunya.

DPP amesema Novemba 25 mwaka huu, askari polisi hao wawili walikamata mzigo wa madini ya dhahabu iliyokuwa ikitoroshwa na wafanyabiashara wakubwa wa madini ambao ni Ally na Nassor.

Amesema mara baada ya kukamata mzigo huo, askari hao polisi waliomba rushwa ya Sh milioni 150 kutoka kwa wafanyabiashara hao wawili wa madini huku wakishirikiana kwa karibu na mchimbaji mdogo wa madini Mtafuni.

“Wafanyabiashara hao wa madini walitoa rushwa ya Sh milioni 150 kwa maofisa hao wa polisi na kisha wakarejeshewa mzigo wa madini hayo ya dhahabu; mzigo huo wa madini ulikuwa unatoroshwa nje ya nchi na haukuwa na vibali vyovyote wala kulipiwa tozo za Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura 123 Marejeo 2019,”alisema Mganga.

Akaongezea “Askari hao wa polisi pamoja na wafanyabiashara tajwa, walijiingiza kwenye genge la uhalifu kwa lengo la kuhujumu uchumi wa nchi, kutoa na kupokea rushwa ili kujilimbikizia mali kinyume na Katiba ya Nchi na sheria zilizowekwa.”

Mganga amesema baada ya kujiridhisha na ushahidi wa awali uliokusanywa na kwa kuzingatia misingi iliyoainishwa kwenye Ibara ya 59B(4)(a) hadi (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na vifungu vya 8 na 9(1)(a) vya Sheria ya Usimamizi wa Mashtaka Sura 430 Marejeo 2019, ameidhinisha mashtaka sita dhidi ya watuhumiwa.

Aliyataja mashtaka yanayowakabili watuhumiwa hao kuwa ni pamoja na kujihusisha na uhalifu wa kupangwa kinyume na Sheria ya Kuzuia Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa kupangwa Sura 200 Marejeo 2019 na kupokea rushwa kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa Sura 329 Marejeo 2019.

Mashtaka mengine yanayowakabili ni kutoa rushwa kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura 329 Marejeo 2019, matumizi mabaya ya nafasi kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura 329 Marejeo 2019 ikisomwa pamoja na Sheria ya Kuzuia Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa Sura 200 Marejeo 2019.

Amesema watuhumiwa hao pia wanakabiliwa na mashtaka ya usafirishaji madini bila kibali kinyume na Sheria ya Madini Sura 123 Marejeo 2019 na utakatishaji wa fedha haramu kinyume na Sheria ya Kuzuia Utakatishaji Fedha haramu Sura 423 Marejeo 2019.

Chanzo: habarileo.co.tz