Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi wawasaka waliovunja na kuiba baa

Polisi Wawasaka Waliovunja Na Kuiba Baa.jpeg Polisi wawasaka waliovunja na kuiba baa

Fri, 3 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala jijini Dar es Salaam linamsaka Godfrey Chacha na genge lake kwa tuhuma za kufanya uhalifu wa kuvunja baa ya Big Mountain iliyopo Banana Ukonga na kuiba mali zinazodaiwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh.milioni 100.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Kamanda wa Polisi mkoa wa kipolisi Ilala Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Debora Magiligimba amesema jeshi hilo linamtafuta kwa nguvu zote mahali popote pale alipo ili akamatwe na Sheria ichukue mkondo wake.

“Hakuna mhalifu yeyote anayeweza kulikimbia Jeshi la Polisi na kama amekimbia, popote pale alipo ajisalimishe haraka kituo chochote cha polisi kwani hawezi kuwa salama atatiwa nguvuni tu,"amesema ACP Magiligimba.

Ameongeza kuwa “Jeshi la Polisi lina mkono mrefu kwanamna yoyote ile tutamkamata na kwamba mtuhumiwa huyo anatafutwa kwa RB namba STK/RB/12887/2022, kwa kosa la kuvunja, kuharibu na kuiba mali.

Kijana huyo baada ya kupata taarifa kuwa alioshirikiana nao kwenye uhalifu huo wamekamatwa na jeshi la polisi inadaiwa kuwa amekimbilia mkoani Mara kwenye wilayani Serengeti na kujificha huko kwa lengo la kukwepa mkono wa sheria ambapo hadi leo hajakamatwa.

Godfrey Chacha kwa kushirikiana na Michael Chacha, Elizabeth Kiguha, Joseph Nyagare na Ester Kamando usiku wa kuamkia Desemba 28, 2022 wanadaiwa waliendesha zoezi la kuvunja baa ya Big Mountain.

Waliokamatwa hadi sasa ni Joseph Nyagare, Michael Julius Chacha, Amosi Chacha na Elizabeth Kiguha.

Hayo yamekuja siku chache baada ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kulitaka Jeshi hilo nchini kufanya kazi kwa weledi ili kuepuka kunyooshewa vidole na wananchi hasa walalahoi.

Rais Dkt.Samia alisema jeshi la polisi ni miongoni mwa taasisi za utoaji haki nchini ambayo inalalamikiwa na wananchi juu ya rushwa kwa kupindisha haki na kuchepusha sheria.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live