Dar es Salaam. Jeshi la Polisi wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, Tanzania limesema linawashikilia wanachama watatu wa ACT-Wazalendo na mwandishi wa habari kwa tuhuma za kufanya maandamano bila kibali.
Jana Jumamosi Agosti 24, 2019 polisi walizuia mkutano wa ndani wa chama hicho uliokuwa ufanyike wilayani humo.
Waliokamatwa ni katibu wa uadilifu, Mbarala Maharagande; mwenyekiti wa jimbo la Ilala, Mwikizu Mayama; mwenyekiti wa chama hicho Temeke, Said Mohammed na mwandishi wa habari wa televisheni mtandao ya Gillybon, Haruna Mpaunda.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Agosti 25, 2019 Kamanda wa Polisi wilayani humo, Amoni Kakwale amesema waliokamatwa walikuwa wakiongoza maandamano bila kuwa na kibali.
"Kama unataka taarifa zaidi unaweza kufika ofisini mimi nakupa taarifa kama msemaji, waliokamatwa walikuwa wakifanya maandamano kinyume na sheria,” amesema Kakwale.
Alipoulizwa sababu za kukamatwa kwa mwandishi wa habari amesema hawezi kutofautisha mwandishi na mwanachama, wote wanahojiwa kwa kosa moja.
Pia Soma
- Alichokisema Waziri Lugola kuhusu wakimbizi wa Burundi
- Kim Jong Un asimamia tena jaribio la kombora
- Hong Kong yazidi kufukuta, waandamanaji waendelea kushinikiza demokrasia
Katibu wa oganaizesheni na mafunzo wa chama hicho, Sheweji Mketo amesema wanaendelea kufuatilia ili wanachama wao wapatiwe dhamana.
Kabla ya mkutano huo kuzuiwa baadhi ya viongozi waliokuwa wamefika ni mshauri mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.