Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi wasimulia walivyomuokoa mtoto ‘kininja’

89572 POLIS+PI Polisi wasimulia walivyomuokoa mtoto ‘kininja’

Mon, 23 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Ni kama sinema. Ndivyo unavyoweza kusema ukisikiliza simulizi ya askari wa Jeshi la Polisi walioshiriki tukio la kumkamata Benson Bernard (31) akiwa ndani ya maji na mwanaye, Goodchance wakiwa watupu, ambapo inadaiwa alitaka kumuua mtoto huyu mwenye miaka saba.

Tukio hilo lilitokea Alhamisi iliyopita saa 12 jioni katika maporomoko ya maji ya Mto Morogoro eneo la Nguzo Campsite, kwa mujibu wa ufafanuzi uliotolewa jana wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa.

Bernard, mkazi wa Kihonda akiwa na mwanaye walikutwa wakiwa watupu huku mtuhumiwa akiwa ameshika panga na msumeno.

Mkewe Mary Shao alieleza jinsi mumewe alivyoanza kuwa na tabia na mwenendo ambao hakuuzoea kuanzia Novemba 29, mwaka huu huku akishukuru kwa mwanaye kupatikana akiwa hai.

Kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, mmoja wa askari walioshiriki kumuokoa mtoto huyu alisema walipokea taarifa kutoka kwa raia wema kwa njia ya simu kwamba baba huyo alionekana kwenye mto huo na mtoto wake wakiwa watupu huku akiwa na panga na msumeno.

“Tulikwenda haraka na kumkuta akiwa amembeba mtoto wake akiwa katikati ya maji yaliyokuwa yakienda kwa kasi na baada ya kumtaka atoke alikaidi amri hiyo na kuanza kuongea maneno yasiyoeleweka ya kikabila, hatukuelewa anaongea lugha gani,” alisema polisi huyo.

Alisema baada ya kumlazimisha alianza kusogea kwenye kina kirefu na kuanza kumzamisha mtoto huyo.

“Baba huyo pia alijaribu kujizamisha na ndipo tulipojitosa ndani ya kina hicho kirefu cha maji na kuanza kupambana naye ili kumuokoa mtoto.

“Jamaa alikuwa na nguvu sana na kwa kuwa alikuwa hana nguo tulipata tabu sana kumdhibiti kwa sababu kila tukimshika alikuwa anateleza.

“Unajua lengo letu ilikuwa kumuokoa mtoto kwanza hata hivyo tulifanikiwa kumkamata baba kisha tukamtoa mtoto,” alisema askari huyo, ambaye hakutaka kutajwa jina lake.

Alisema walipotolewa kwenye maji wote wawili walipewa huduma ya kwanza.

“Walitapishwa maji, ikatulazimu kumsitiri huyu bwana (Bernard) kwa kumpatia nguo na kupelekwa kituo cha polisi.”

Akisimulia huku akitabasamu alisema, “simu, saa, viatu vyetu viliharibika baada ya kujitosa kwenye maji kuwaokoa. Hatukujua kama angechukua uamuzi wa kujizamisha kwenye maji pamoja na mtoto. Tulipata ujasiri bila kujali tulivaa nini.”

Bernard alitambuliwa kuwa anafanya kazi katika kiwanda cha ufundi uashi kilichopo mtaa wa Sabasaba kata ya Mbuyuni mjini Morogoro.

Juma Ramadhani, ambaye anamfahamu Bernard alieleza kuwa wiki mbili zilizopita alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa.

“Alikuwa akiongea vitu tofauti huku akidai kuwa yeye ni mfalme wa vitu vyote vilivyopo hapa duniani ikiwemo mito na milima,” aliongeza Ramadhani.

Alisema kuwa baada ya kuona hali hiyo yeye na wenzake walizungumza na familia yake ili wampeleke hospitali.

“Kabla ya kufanya uamuzi huo wa kumpeleka hospitali ndugu yake kutoka Singida alikuja na kutaka kumpeleka hospitali. Ila alipofika tu Bernard alirejea katika hali yake ya kawaida na kuendelea na kazi na ndugu yake huyo alirudi Singida,” alisema Ramadhani.

Alisema baadaye mwenzao huyo hali yake ilibadilika na kurejea kuzungumza vitu visivyoeleweka.

“Mara nyingi alihoji kwanini watu wanaishi kwenye milima ambayo ni mali yake. Tulimshauri mkewe kumpeleka hospitali lakini ilishindikana. Ninamfahamu Benson miaka miwili iliyopita, kwa kipindi chote sijawahi kumuona akitumia kilevi wala kugombana na mtu,” alisimulia Ramadhani.

Alichokisema mkewe

Mary alisema mumewe alianza kubadilika tabia na mwenendo kuanzia Novemba 29.

“Alikuwa akizungumza mambo yasiyoeleweka kuhusu ufalme wa mbinguni. Tuna watoto wawili na hatukuwahi kuwa na ugomvi. Yeye (Bernard) hajaokoka, alipoanza kuongea maneno ya ufalme wa mbinguni nilishtuka.”

Alisema siku ya tukio alimchukua mtoto akiaga kuwa wanakwenda kuogelea.

“Baadaye nilipigiwa simu na kuelezwa amekutwa akitaka kumzamisha mtoto kwenye kina cha maji,” alisema.

Kamanda wa Polisi

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana, Mutafungwa alisema wakati polisi wakiendelea na uchunguzi, madaktari wa kitengo cha afya ya akili nao wanamchunguza Bernard.

“Pamoja na kufanya tukio hilo, Bernard alikatakata mabomba kwenye chanzo cha maji ya mto,” alisema Mutafungwa.

Mutafungwa alisema walipata taarifa kutoka kwa raia wema waliomtilia shaka mtuhumiwa huyo baada ya kuonekana kwenye eneo hilo akiwa mtupu na mwanaye.

Chanzo: mwananchi.co.tz