Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi waokoa viongozi wa Wamachinga Dar

8c9cbe2f90c5ccfc8328ab1fbaf5389f.jpeg Polisi waokoa viongozi wa Wamachinga Dar

Wed, 20 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwaokoa viongozi wa wafanyabiashara wadogo maarufu Wamachinga katika Mtaa wa Msimbazi jijini humo.

Makalla amesema zilitokea vurugu jana wakati viongozi hao wa Wamachinga walipokuwa wakiunga mkono jitihada za serikali kuwapanga wafanyabishara hao pamoja na kuwatoa walioziba njia za watembea kwa miguu.

Aliwapongeza viongozi wa Wamachinga mkoa wa Dar es Salaam kwa kazi nzuri waliyoifanya na akawatia moyo kuwa wameonesha ukomavu na wameelewa nia nzuri ya serikali.

“Na nilipongeze Jeshi la Polisi kwa kuwahi kwa haraka kwenda kuwaokoa viongozi wa Wamachinga wakati wanatimiza majukumu yao,” alisema Makalla.

Aliwaeleza wafanyabiashara hao kuwa serikali ipo katika mpango wa kuwaweka sawa na katika mwezi mmoja uliotolewa ilitolewa elimu na juzi aliongeza siku 12 kwa Wamachinga hao waondoke kwenye maeneo yasiyo rasmi.

Makalla alisema atakuwa akienda maeneo ya Kariakoo mara kwa mara kuhakikisha wafanyabiashara hao wanatekeleza agizo hilo.

“Leo (juzi) ni mwisho tarehe 18, mimi nitamwomba radhi Waziri Mkuu aniruhusu mpaka tarehe 30 mwezi huu. Sasa hivi katika kufuatilia hili nitaelekeza nguvu Kariakoo. Nataka kujua mmesikia au hamjasikia kwa kuwa maeneo yapo,” alisema na kuongeza:

“Baada ya kuongeza siku hizo 12, nataka kusikia wafanyabiashara wakisema wamekosa maeneo hivyo watafutiwe mengine kwa kuwasumbua wakuu wa wilaya na si kubaki katika maeneo yasiyoruhusiwa.”

Makalla alisema anataka kuzungumza na uongozi wa shirika la DDC Kariakoo aone kama kuna uwezekano wa kuwaweka baadhi ya wafanyabiashara katika eneo hilo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz