Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi wanne waliofukuzwa kazi wapandishwa kizimbani

31309f84eca9123771e5f3f3a5ffa6ae Polisi wanne waliofukuzwa kazi wapandishwa kizimbani

Thu, 14 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

ASKARI watatu waliofukuzwa kazi hivi karibuni pamoja na raia watano wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha wakikabiliwa na mashitaka sita yakiwamo ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kupanga njama za kujipatia fedha Sh milioni 10 kati ya milioni 30 kutoka kwa mfanyabiashara, Sammy Mollel.

Aidha, askari mwingine Koplo William Joseph (44) na mkewe Dorcas Michael (32) wamepandishwa kizimbani kujibu mashitaka matano likiwemo la uhujumu uchumi na kukutwa na misokoto 20 ya bangi.

Waliofikishwa pia katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha ni mfanyabiashara wa madini ya tanzanite jijini Arusha, Lucas Mdeme (46) mkazi wa Njiro jijini hapa.

Askari watatu waliofukuzwa kazi kwa tuhuma ya rushwa na kupandishwa kizimbani jana ni Heavenlight Mushi aliyekuwa askari Kitengo cha Intelijensia Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Dar es Salaam, Konstebo Gasper Paul wa Kitengo cha Intelijensia Makao Makuu Dodoma na Konstebo Bryton Murumbe, askari wa kawaida mkoani Dodoma.

Raia wengine waliopandishwa kizimbani ni Joseph Chacha (43) mkazi wa Ilboru, Leonila Joseph (46) mkazi wa Ilboru, mfanyabiashara Nelson Lyimo (58) wa Kijenge Juu, na Omary Alphonce (43) mkazi wa Olasiva, wote wa Arusha.

Waendesha mashitaka waandamizi wa serikali, Adelaide Kassalay na Agnes Hyera mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Arusha, Rose Ngoka walidai katika shitaka la kwanza linawakabili mshitakiwa wa kwanza, wa pili na watatu ambao ni askari hao wa zamani kuwa Desemba 5, mwaka jana walijihusisha na uhalifu huku wakitambua kuwa wao ni watumishi wa umma na kujipatia rushwa ya awali ya Sh milioni 10 kutoka kwa Sammy Mollel.

Mollel ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Gems & Rock Venture ya jijini Arusha. Kassalay alisoma shitaka la pili linalowakabili washitakiwa wanne ambaye ni Chacha, wa tano Joseph, wa sita Lyimo, wa saba Mdeme na wa nane Alphonce, wote wanashitakiwa kwa kujifanya watumishi wa umma na kuunda mtandao wa kihalifu na kupanga njama za kujipatia fedha taslimu Sh milioni 10 kutoka kwa Mollel.

Mwendesha mashitaka huyo alisoma shitaka la tatu linalowakabili watuhumiwa wote nane ambalo ni la kupanga njama za kuhujumu uchumi kuwa Desemba 5, mwaka jana walijipatia fedha Sh milioni 10 kutoka kwa Mollel.

Alisema shitaka la nne linamkabili Chacha ambaye anatuhumiwa akiwa na nia alifanya uhalifu na udanganyifu na kujitambulisha kuwa yeye ni mtumishi wa umma akifanya kazi Ikulu.

Mwendesha mashitaka huyo alisoma shitaka la tano linalowahusisha washitakiwa wote kwa kufanya udanganyifu na kujipatia fedha kiasi cha Sh milioni 10 za awali kati ya milioni 30 ili wamwachie huru kwa tuhuma za kukwepa kodi na kufanya biashara ya madini ya tanzanite kwa kutorosha madini nje kinyume cha sheria.

Kassalya alisoma shitaka la sita la utakatishaji fedha haramu linalowakabili washitakiwa wote akidai wote kwa pamoja Desemba 5, mwaka jana walipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Sh milioni 10 kutoka kwa mfanyabiashara Mollel.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, Hakimu Ngoka aliwaeleza watuhumiwa kuwa hawatakiwi kujibu chochote kwani mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza mashitaka hayo na wamerudishwa rumande hadi Januari 27, mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.

Wakati huo huo, katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Arumeru, aliyekuwa askari Polisi, Koplo Joseph (44) mkazi wa Muriet jijini Arusha na mkewe Dorcas wamepandishwa kizimbani kujibu mashitaka matano likiwemo la uhujumu uchumi na kukutwa na misokoto 20 ya bangi.

Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Serikali, Adelaide Kassalay alisoma mashitaka hayo jana mbele ya Hakimu Mfawidhi Mary Mushi.

Katika shitaka la kwanza linalowakabili washitakiwa wote ilidaiwa kuwa Januari tan mwaka huu waliingilia mfumo ugawaji umeme na kujiunganishia nishati hiyo kinyume cha utaratibu na kuhujumu uchumi wa nchi.

Kassalay alisoma shitaka la pili kuwa Januari 5, mwaka huu washitakiwa wote walipatikana na mimea iliyozuiliwa kisheria nyumbani kwao wakati wakijua wazi kuwa mimea hiyo ni dawa za kulevya.

Katika shitaka la tatu linalowakabili washitakiwa wote ilidaiwa kuwa walikutwa na pombe haramu ya gongo lita tano nyumbani kwao Muriet wakati wakifahamu kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Shitaka la nne ni kuwa walitumia alama ya biashara kwa njia ya udanganyifu na kufanya serikali ikose mapato.

Alisema shitaka la tano linalowakabili washitakiwa hao ni kupatikana na vifungashio vya plastiki vilivyopigwa marufuku na serikali mwaka 2018 maarufu kwa jina la viroba nyumbani kwake Muriet jijini Arusha.

Hakimu Mushi aliwaeleza washitakiwa hao kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 27, mwaka huu.

Chanzo: habarileo.co.tz