Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi wamdaka ngariba aliyekuwa akikeketa wasichana Mara

Ukeketajiii Polisi wamdaka ngariba aliyekuwa akikeketa wasichana Mara

Tue, 9 Aug 2022 Chanzo: Dira Makini

Jeshi la Polisi mkoani Mara linamshikilia Ngariba aitwae Rhobi Mahando Magoko (50) maarufu kwa jina la Mokehanga ambaye ni Mkazi wa Kebanchabancha Wilaya ya Serengeti na Kijiji cha Nyabisaga Kata ya Sirari Wilaya ya Tarime akidaiwa kujihusisha na kitendo cha kuwakeketa wasichana huku akihama hama katika maeneo mbalimbali mkoani humo.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 9, 2022 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Longinus Tibishubwamu na kusema kuwa, mtuhumiwa huyo amekuwa akijishughulisha na kitendo cha kuwakeketa wasichana huku akihama hama kitendo ambacho ni kinyume cha sheria za nchi.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa na Polisi Agosti 4, 2022 Kijiji cha Nyabisaga Wilaya ya Tarime na kupelekwa Mugumu Wilaya ya Serengeti ambapo mpaka sasa anashikiliwa na kwamba, baada ya upelelezi na taratibu zote kukamilika atafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.

"Ni kweli mtuhumiwa huyo anashikiliwa kwa kujihusisha na ukeketaji wa mabinti na baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani, anaonekana amekuwa akifanya hazi hiyo kwa muda mrefu kwa kuhama hama nitoe wito kwa wazazi na walezi wasiwakekete watoto wao wa kike, kwani ukeketaji una madhara mengi ikiwemo maumivu makali wakati wa kukeketwa hali ambayo inaweza kupelekea kifo na madhara mengine mengi yakiwemo magonjwa ya kuambukiza kutokana na kutumia kifaa kimoja wakati wa ukeketaji,"amesema.

Aidha, Kamanda Tibishubwamu ameongeza kuwa,Serikali haitawafumbia macho wanaojishugulisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia na amewataka wananchi kutoa taarifa mapema polisi na katika ofisi za serikali pindi wanapoona mtu yuko katika maandalizi ya kukeketa ama kufanya vitendo ambavyo ni kinyume cha sheria.

Daniel Misoji ambaye ni Mkuu wa Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama kinachomilikiwa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, shirika ambalo hujishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutetea haki za binadamu lenye makao make yake Mugumu Wilayani Serengeti amesema, mpaka sasa kituo hicho (Hope Mugumu) kimepokea wasichana 32 kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Serengeti waliokimbia ukeketaji kutoka katika familia zao na wanapatiwa hifadhi kituoni hapo.

"Tumepokea mabinti 32 waliokimbia ukeketaji kutoka katika familia zao kutokea maeneo mbalimbali ya Serengeti ikiwemo Nyamoko, Machochwe, Rung'abure na Kebanchabancha. Bado tunaendelea kupokea, nisema tu kwamba hiki ni kipindi cha likizo wapo wazazi na walezi wanatumia huu mwanya wa likizo kuwakeketa mabinti niwaombe waache.Ukeketaji haufai, sote kwa pamoja tuungane kuutokomeza," amesema Misoji.

"Tuwafichue mbele ya vyombo vya sheria wale wote ambao wana mpango wa kuwafanyia ukeketaji mabinti kabla hawajafanya tuweze kudhibiti mapema, kwa sababu wapo katika jamii tunaishi nao.

"Mwaka huu unagawanyika kwa mbili kwa hiyo ukeketaji utafanyika kwa kiwango kikubwa, lakini tukiunganisha nguvu kwa pamoja tutaweza kudhibiti taarifa zitolewe Polisi haraka, Ofisi za serikali za vijiji, ofisi za maendeleo ya Jamii na kwa watu wa kuaminika ambao ni haraka kuchukua hatua wakifahamishwa,"amesema Misoji.

Pia, amewaomba watu wanaofanya kazi hiyo ya kukeketa (Ngariba) kama njia ya kujipatia kipato waache mara moja kazi hiyo, bali watumie njia halali ambazo zinakubalika kisheria kujipatia kipato. Huku akiwahimiza wazee wa Kimila wilayani Serengeti kuwa sehemu muhimu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuumaliza ukeketaji kwa kutoa matamko ya kukemea mila hiyo.

"Zipo kazi za kufanya ikiwemo kilimo, biashara, ufugaji na ushonaji mtu akizifanya kwa ufanisi anaweza kufanikiwa kimaisha badala ya kukeketa kwani mwisho wake ni mbaya,"amesema Misoji.

Chanzo: Dira Makini