Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi walituhumiwa kuhusika na vifo watu waliofia mikononi mwao

32529 Vifo+pic Tanzania Web Photo

Thu, 20 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwaka 2018 unaelekea ukingoni wakati Jeshi la Polisi likiwa limebebeshwa mzigo wa tuhuma za mauaji ya raia, ama kwa kupigwa risasi au kufia katika vituo vyake kutokana na vipigo.

Jeshi hilo lilijikuta pia katika lawama kwa kuendelea kujichunguza lenyewe dhidi ya tuhuma hizo na kila mara kuishia kujisafisha badala ya kuacha vyombo huru kutafuta ukweli wa matukio hayo.

Matukio hayo yalisababisha baadhi ya ndugu wa marehemu kususia miili ya wapendwa wao na wale waliokubali kuchukua walifanya hivyo shingo upande.

Kifo cha Kapange

Siku zaidi ya 170 mpaka jana, ndugu wa marehemu Frank Kapange, mkazi wa Mbeya na mfanyabiashara wa mitumba aliyedaiwa kufia mikononi mwa polisi Juni 4 wamesusa kuchukua mwili wake wakitaka uchunguzi huru.

Hilo linatokea licha ya Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya kutupilia mbali rufaa yao walikoomba itengue uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya ya kutupa ombi lao la kutaka uchunguzi wa kina kuhusu kifo cha ndugu yao.

Kifo kama hicho kinadaiwa kumpata pia Allen Mapunda (22), kwani Machi 25 wakazi wa Kata ya Iyela, Mbeya walizusha tafrani mitaani wakihoji kifo cha kijana huyo kilichotokea muda mfupi baada ya kuachiwa kutoka Kituo Kikuu cha Polisi alikokuwa akishikiliwa.

Mfululizo wa malalamiko ya watu kudaiwa kuuawa na polisi ulishika kasi baada ya kuuawa kwa Akwilina Akwilini, aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Dar es Salaam.

Akwilina alipigwa risasi akiwa ndani ya daladala lililokuwa likitokea Mabibo kuelekea Makumbusho baada ya kutokea vurugu kati ya polisi na wafuasi wa Chadema Februari 16 katika eneo la Mkwajuni, Kinondoni.

Wafuasi hao wa Chadema walikuwa wakiandamana kuelekea ofisi za Manispaa ya Kinondoni kushinikiza mkurugenzi mtendaji atoe barua za utambulisho wa mawakala wao wa kusimamia uchaguzi ambaohadi siku ya mwisho ya kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Kinondoni walidaiwa kuwa hawakuwa wamepewa.

Baada ya mauaji hayo, polisi ilikiri kuwasambaratisha viongozi na wafuasi wa Chadema, lakini ilidai kuwa askari wake walikuwa wakirusha risasi hewani.

Jeshi hilo pia lilikiri kuwashikilia askari wake sita kuwahoji kuhusu tukio hilo na Aprili 20, mkurugenzi wa mashtaka (DPP), Biswalo Mganga aliwaambia wanahabari kuwa amefunga rasmi jalada la kesi hiyo.

Mganga alisema Jeshi la Polisi linapotumia nguvu kuzuia maandamano haliwezi kushtakiwa au hata kukitokea vurugu na kusababisha mauaji.

Baadaye viongozi watano wa Chadema akiwamo mwenyekiti wao, Freeman Mbowe waliitwa Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na kuhojiwa kisha kushtakiwa kwa kuhamasisha maandamano, uchochezi na uasi. Kesi hiyo bado ipo mahakamani.

Tukio jingine ni la kifo cha Andrew Kiwia aliyekuwa dereva wa Toyota Hiace na mkazi wa Mnazi Moshi mkoani Kilimanjaro aliyefia katika mahabusu ya Kituo Kikuu cha Polisi wilayani humo akidaiwa kufa katika jaribio la kujinyonga.

Familia yake haikukubaliana na maelezo hayo huku wakidai kuwa maiti ilikuwa na jeraha kichwani lililosababishwa na kipigo cha askari.

Andrew alikamatwa Septemba 26 na askari waliokuwa doria saa tano asubuhi akiwa na mwenzake, Obasanjo Kitwi jirani na stendi ya Kiborloni na kupelekwa polisi.

Vyanzo kutoka ndani ya polisi vilidai kuwa kijana huyo na mwenzake walikamatwa wakiwa na pombe aina ya gongo, lakini ndugu walipinga taarifa hiyo wakidai alikamatwa wakati akimnyoa nywele Obasanjo na taarifa za kifo hicho zilijulikana asubuhi ya siku iliyofuata.

Jeshi la Polisi halikueleza mtuhumiwa huyo aliwezaje kujinyonga kwa kutumia suruali yake aina ya jeans akiwa mahabusu bila wenzake kushuhudia na kutoa taarifa kwa polisi wa zamu.

Akizungumzia tukio hilo, kaka wa marehemu, Frank Kiwia alidai kuwa alipouchunguza mwili wa mdogo wake aliona paji la uso likiwa limepasuka na mikono ilikuwa na majeraha makubwa.

Mauaji mengine yaliyolalamikiwa dhidi ya polisi yalitokea Aprili 27, Suguta Chacha (27) alifariki dunia akiwa mikononi mwa polisi na Julai 27, mkazi wa Kijiji cha Rubambagwe wilayani Chato mkoani Geita, Pascal Kanyembe (39) alifariki akiwa mikononi mwa polisi baada ya kukamatwa.

Oktoba 21 kulitokea mauaji wilayani Uvinza mkoani Kigoma ambapo askari polisi watatu akiwamo mkuu wa Kituo cha Polisi cha Nguruka, Uvinza, Ramadhan Mdimi waliuawa kwa kupigwa na silaha za aina mbalimbali za jadi ikiwamo mishale wakati wakitekeleza majukumu yao pembezoni mwa mpaka wa kijiji cha Mpeta.

Mauaji hayo yalitokana na mgogoro wa ardhi katika eneo la Ilunde na askari hao walifika kuwaondoa wananchi eneo hilo walioanzisha makazi na kufanya shughuli za kilimo pamoja na ufugaji bila kufuata sheria na taratibu za ardhi tangu mwaka 2004.

Oktoba 28, 2018, mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam akidai kuwa zilikuwa zimepita siku 10 na kwamba yalitokea mauaji ya watu zaidi ya 100, wakiwamo polisi.

Hata hivyo, taarifa hiyo ilikanushwa na Jeshi la Polisi na baadaye kiongozi huyo wa ACT Wazalendo alishikiliwa na jeshi hilo jijini Dar es Salaam tangu Oktoba 31 kabla ya kufikishwa mahakamani Novemba 2, 2018.

Kauli ya Serikali

Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi, siku chache tangu ateuliwe kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alisema bado hajapokea ripoti ya uchunguzi wa matukio ya namna hiyo ambayo yamethibitisha kuwa mtu amekufa kwa kipigo cha polisi.

“Ukweli wa mambo haya una uhusiano na majibu ya postmoterm (uchunguzi wa kitabibu wa sababu ya kifo), mimi sijapata tukio la mtu alikufa kituoni na ikathibitisha tumegundua alipigwa na polisi,” alisema Lugola.

“Kwa hiyo hili suala ni gumu kulisemea wakati hakuna tukio lililothibitishwa na uchunguzi.”

Alipoulizwa ni kwa nini sheria ya vifo vyenye utata isitumike badala ya polisi wanaotuhumiwia kuunda timu ya uchunguzi, Lugola alisema: “Kila tukio likitokea lenyewe kwa nature (asili) yake litatuongoza cha kufanya. Si kila tukio linashughulikiwa sawa na jingine. Matukio hayafanani, kwa hiyo huwezi kuwa na fomula moja.”

Hata hivyo, akijibu swali la Khatib Said Haji bungeni Septemba 13, Lugola alisema kifo ni mtego unaomnasa mtu wakati wowote na mahali popote.

“Kwa hiyo mwananchi anaweza kufa akiwa polisi, akiwa anafanya mapenzi, anaweza akafa akiwa kwenye gari anasafiri na aweza kufia hata humu ndani bungeni. Isije ikachukuliwa kwamba aliyefia kituo cha polisi huwa ameteswa,” alisema Lugola.



Chanzo: mwananchi.co.tz