Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi waliotimuliwa wadaiwa kukiri rushwa mil 30/-

69df47564006ccc588d3dafe0084270e Polisi waliotimuliwa wadaiwa kukiri rushwa mil 30/-

Thu, 11 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WASHITAKIWA wanane wakiwemo askari polisi watatu waliofukuzwa kazi kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh milioni 30, wanadaiwa kukiri kosa na wamemwandikia Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuhusu suala hilo.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni raia watano akiwemo mfanyabiashara wa madini ya tanzanite jijini Arusha, Lucas Mdeme.

Mmoja wa mawakili wa washitakiwa hao, Charles Kagirwa, jana aliieleza Mahakama kuwa, wateja wao wote wamekiri kosa hivyo wamemuandikia barua DPP kuhusu washitakiwa hao kukiri makosa na wanasubiri majibu.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka sita likiwemo la uhujumu uchumi, utakatishaji fedha haramu na kupanga njama za kujipatia rushwa ya fedha ya awali Sh milioni 10 kati ya Sh milioni 30 walizohitaji kutoka kwa mfanyabiashara ambaye pia ni Mweyekiti wa Chama Cha Wauzaji Madini Wakubwa Ndani na Nje (TAMIDA), Sammy Mollel.

Waendesha mashitaka wa serikali, Adelaide Kassalay na Agnes Hyera, walimweleza Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Rose Ngoka, kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo, wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.

Walisema hawajapewa taarifa rasmi kuwa washitakiwa wameandika barua kwa DPP kukiri makosa.

Hakimu Ngoka aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 24 na akawaeleza washitakiwa kuwa wataendelea kukaa rumande kwa kuwa Mmahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Waliopandishwa kizimbani baada ya kufukuzwa kazi aliyekuwa askari mwenye namba G. 5134 DC Heavenlight Mushim, aliyekuwa askari Kitengo cha Intelijensia Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Dar es Salaam, H. 125 PC Gasper Paul wa Kitengo cha Intelijensia Makao Makuu Dodoma, na H.1021 PC Bryton Murumbe, aliyekuwa askari wa kawaida mkoani Dodoma.

Washitakiwa wengine ni Joseph Chacha na mfanyabiashara Leonila Joseph mkazi wa Ilboru, Mkazi wa Kijenge Juu, Nelson Lyimo na mkazi wa Olasiva jijini Arusha, Omary Alphonce.

Mahakama ilielezwa kuwa shitaka la kwanza linawakabili mshitakiwa wa 1,2,3 ambao ni askari ni kuwa, Desemba 5 mwaka jana walijihushisha na uhalifu huku wakitambua kuwa wao ni watumishi wa umma na kujipatia rushwa ya awali Sh milioni 10 kutoka kwa Sammy Mollel ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Gems & Rock Venture ya jijini Arusha.

Shitaka la pili linawakabili washitakiwa wanne ambao ni Chacha Joseph, mshitakiwa wa tano, mshitakiwa wa sita Lyimo, mshitakiwa wa saba ni Mdeme na mshitakiwa wa nane ni Alphonce.

Wanashitakiwa kwa kujifanya watumishi wa umma na kuunda mtandao wa kihalifu na kupanga njama za kujipatia fedha Sh milioni 10 kutoka kwa Mollel.

Shitaka la tatu linalowakabili watuhumiwa wote ni la kupanga njama za kuhujumu uchumi, kwamba, Desemba 5 mwaka jana walijipatia Sh milioni 10 kwa Mollel.

Shitaka la nne linamkabili Chacha anayetuhumiwa kuwa, akiwa na nia kufanya uhalifu na udanganyifu, alijitambulisha kuwa yeye ni mtumishi wa umma, ikulu.

Katika shitaka la tano washitakiwa wote wanadaiwa kufanya udanganyifu na kujipatia Sh milioni 10 za awali kati ya Sh milioni 30 ili wamwachie huru kwa tuhuma za kukwepa kodi na kufanya biashara ya madini ya tanzanite kwa kutorosha madini.

Shitaka la sita la utakatishaji fedha haramu linawakabili washitakiwa wote wakiwadaiwa kuwa, kwa pamoja Desemba 5 mwaka jana, walijipatia Sh milioni 10 kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa mfanyabiashara, Sammy Mollel.

Chanzo: habarileo.co.tz