Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi wakubali uchunguzi kifo wanachohusishwa nacho

56940 Pic+polisi

Tue, 14 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma.Hatimaye jeshi la polisi mkoani Dodoma limekubali kufanyika kwa uchunguzi (post mortem) wa mwili wa kijana Hillary Shirima (19) ambaye ndugu zake wanadai amukufa kutokana na kipigo cha askari wa jeshi hilo.

Gazeti hili jana liliripoti kuhusu kifo chenye utata cha kijana huyo aliyefariki Mei 2 baada ya kukaa hospitali kwa siku mbili na tangu wakati huo ndugu zake wamegoma kuuchukuwa mwili uliohifadhiwa katika hospitali ya mkoa wa Dodoma ambao leo unatimiza siku ya 11 wakishinikiza ufanyiwe uchunguzi.

Ndugu wa marehemu wanadai kijana huyo alikufa kutokana na kipigo akiwa mikononi mwa polisi huku majirani wakimtaja mwajiri wake kuhusika na kipigo hicho.

Jana baba mdogo wa marehemu, Zubery Joseph aliliambia Mwananchi kuwa wamepata kile walichokuwa wanahitaji hivyo wanasubiri uchunguzi huo ufanyike ili waanze maandalizi ya kumzika ndugu yao.

Shirima alifikishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma Aprili 29 akiwa na hali mbaya inayoelezwa kutokana na kipigo huku akiwa amefungwa pingu na kusindikizwa na polisi lakini usiku wa kuamkia Mei 2 alifariki dunia.

“Awali tulipanga kutokuuchukua mwili huo kabisa kama Serikali isingekubali kufanyika uchunguzi ambao na sisi tutakuwa na mwakilishi.”

Pia Soma

“Kamanda (kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma) alitupa maelekezo lakini tukaenda hadi kwa Mkuu wa wilaya, leo (jana) tutafanya uchunguzi na sisi ndugu tunakuwa na mwakilishi wetu hapo hivyo baada ya hapo sisi tutaendelea na taratibu za mazishi kusubiri taarifa yao,” alisema Joseph.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alisema jeshi hilo litatoa ushirikiana katika uchunguzi huo na yeye atakuwa karibu na wahusika.

“Kila hatua nitafuatiliana, lengo hapa ni kuondoa utata ambao unaweza kujitokeza na watu kutokuaminiana, hakutakuwa na kificho wala upendeleo katika jambo zito kama hilo,” alisema Kamanda Muroto.

Chanzo: mwananchi.co.tz