Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi waingilia kati kifo cha utata

00dcbf5ac1c5cb68ad2fb0ae055a5a78.jpeg Polisi waingilia kati kifo cha utata

Thu, 20 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JESHI la Polisi Mkoani Mwanza limeingilia kati mazishi ya Denis Mathias (20) mkazi wa Mtaa wa Buzuruga Kaskazini katika Manispaa ya Ilemela anayedaiwa kupigwa na kufia katika Kituo cha Afya Buzuruga alipokuwa anapatiwa huduma ya matibabu.

Akizungumza na HabariLEO jana katika Makaburi ya Buzuruga Mashariki, mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza, Aloyce Kessy, alisema baadhi ya vijana walichukua mwili wa marehemu nyumbani kwa marehemu na kuupeleka Ofisi ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyambiti, Manispaa ya Ilemela wakitaka uongozi wa ofisi hiyo umzike marehemu kwa madai ndio waliosababisha kifo hicho.

Kessy alisema vijana hao walikwenda makaburini hapo na kufukia kaburi lilokuwa limechimbwa kwa ajili ya kumzika na kuzimisha moto kwenye msiba huo.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo, walifuatilia na kuwaomba waombolezaji kuwa na subira kwani wote wliohusika na kifo hicho watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

“Baada ya kupata taarifa hizo ambazo zingesababisha uvunjifu wa amani, tulifika na kuchukua mwili huo kwenye Ofisi ya Mtaa wa Nyambiti na kuupeleka Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure kufanyiwa uchunguzi na baadaye tukashauriana na familia ya marehemu na hivyo kuja kusimamia mazishi haya,” alisema.

Wananchi waliokuwa na hasira walieleza kuchoshwa na matukio ambayo yamekuwa yakifanywa na viongozi wao wa mtaa ya kujichukulia sheria mikononi na kuomba serikali ikomeshe hali hiyo.

Ivan Jummane anayedai alikuwa na marehemu walipokamatwa siku ya Ijumaa saa nne usiku na Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyambiti akiwa na Kamati ya Ulinzi ya Mtaani hapo, alisema marehemu alipelekwa katika ofisi ya mtaa na kuanza kupiwga kwa kosa la uzururaji na alipozidiwa walimpeleka katika Kituo cha Afya Buzuruga alipofia hapo Mei 15, mwaka huu.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Neema Charles, alisema matukio ya namna hiyo yanajenga picha mbaya katika jamii kwa kuwepo viongozi wasiojali haki ya binadamu kuishi na hivyo, kuomba mamlaka za serikali kuangalia vigezo vya kuwapata viongozi.

Diwani wa Kata ya Buzuruga, Manusura Lusigaliye, alilipongeza Jeshi la Polisi ka kufika katika eneo hilo ya kuhakikisha kazi ya kuzika mwili wa kijana huyo inafanyika kwa amani.

Chanzo: www.habarileo.co.tz