Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi wafunga mtaa Dar usiku, wamnasa mtuhumiwa wa 'unga'

53649 Pic+dawa

Tue, 23 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ilikuwa kama sinema wakati wa msako wa kile kinachodaiwa kuwa dawa za kulevya katika nyumba iliyopo mtaa wa Pemba, eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Tukio hilo lililotokea saa saba usiku wa kuamkia Jumamosi Aprili 20, lilihusisha kikosi cha polisi, ambacho mashuhuda walidai kuwa kilikuwa na takribani askari 30.

Askari hao walitanda mtaani hapo na wengine walionekana wakipanda na kushuka kwenye nyumba hiyo ya ghorofa walikokuwa wakimsaka mtuhumiwa wakiwa na silaha za moto.

Ukamataji huo ulianza kwa askari anayedhaniwa ni wa kitengo cha kudhibiti dawa za kulevya, kumpigia simu mwenye nyumba kwamba wamefika nyumbani kwake na wanahisi mmoja wa wapangaji wake ana mzigo wa dawa hizo ndani.

Jana, Mwananchi lilimtafuta mwenye nyumba huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Hidaya.

Alisema alipigiwa simu na mlinzi wake akimweleza kuwa kuna polisi wamefika wanataka kufanya upekuzi katika ghorofa ya nne anakoishi mtuhumiwa, hivyo walitaka kuzungumza naye.

Hidaya alisema baadaye alipigiwa tena simu na ofisa mmoja wa polisi akimtaka ampe namba ya mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo ili wampatie taarifa na afike nyumbani hapo ashuhudie upekuzi waliotaka kuufanya kwenye chumba anachoishi mpangaji wake anayedaiwa kuwa ni raia wa Congo, naye alitekeleza.

Alisema baada ya maofisa hao kufanya upekuzi alipigiwa tena simu na askari aliyemjulisha kuwa wamemkamata mpangaji wake akiwa na kilo 15 za dawa zinazodhaniwa ni za kulevya.

“Hawa polisi walifanya upekuzi kuanzia saa 7 usiku hadi saa 11 alfajiri,” alisema Hidaya.

Mwananchi lilipotaka kujua kama Hidaya aliwahi kufahamiana na mpangaji huyo kabla hajapanga nyumbani kwake, alikana kumjua akieleza kuwa kwake alipelekwa na madalali wa nyumba na alipokewa na mwanaye wa kwanza.

“Na wala hatukuwa tunafahamu kama anaweza kudhaniwa anajihusisha na biashara ya dawa za kulevya, bali tunachojua ni mfanyabiashara na ana maduka yake Kariakoo anauza nywele za bandia, rasta na mawigi.”

Mkazi anayeishi karibu na ghorofa hilo alisema siku ya tukio alishuhudia magari mawili ya polisi yakiwa na askari zaidi ya 15 ambao walifika eneo hilo na kulizunguka.

Alipotafutwa jana, kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Zuberi Chembela alikiri kukamatwa kwa mtu huyo, lakini alidai suala hilo lipo juu ya uwezo wake na kwamba wanaoweza kulizungumzia ni kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam au Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).

Alipotafutwa na Mwananchi, kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema yuko kwenye kikao.

Mwananchi lilipomtafuta kamishna wa Tume ya Uratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya (DCEA), Rodgers Siyanga alisema watafutwe polisi Kitengo cha Dawa za Kulevya ambao ndio waliomkamata mtu huyo akiwa kwenye nyumba ya kulala wageni.

“Kumbe na wenzetu polisi Kitengo cha Dawa za Kulevya na wao walikuwa wanamtafuta kwa bahati nzuri wamemkamata, hivyo watafute wakupe taarifa,” alisema Siyanga.

Walipotafutwa polisi kitengo hicho walidai watatoa taarifa za kukamatwa mtuhumiwa huyo leo ofisini kwao.

Hivi karibuni Jeshi la Polisi Kikosi cha Viwanja vya Ndege wa Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), lilimkamata raia wa Latvia, Linda Mazure (22) akiwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilo 5.091 alizokuwa akisafirisha kwenda nchini Poland.



Chanzo: mwananchi.co.tz