Polisi mkoa wa Arusha wameendesha operesheni ya kukagua magari ya abiria na mizigo usiku kubaini makosa na uzembe unaoweza hatarisha uhai wa watumiaji wa barabara na wao wenyewe.
Katika operesheni iliyofanyika usiku wa kuamkia leo katika maeneo ya Arumeru mkoani Arusha, askari wa kikosi cha usalama barabarani wamekagua kiwango cha ulevi mwilini kwa madereva, alama za usalama, kiwango cha abiria ndani ya basi na mwendokasi wa magari ya abiria.
Kamanda wa kikosi cha Usalama Barabarani nchini Naibu Kamishna wa Polisi DCP Ramadhan Ng’anzi amesema kuwa kikosi hicho kipo katika mwendelezo wa operesheni ya saa 24 ambayo imelenga kukagua vyombo vyote huku akiweka wazi kuwa wanakagua makosa hatarishi ikiwemo mwendokasi na ubovu wa magari.