Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi waeleza sababu za kukamatwa Bawacha

MULIROOO WEB Kamanda Jumanne Muliro

Sat, 2 Oct 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) wakilalamika kukamatwa kwa wanachama na wafuasi wa baraza hilo leo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum limethibitisha kuwashikilia likidai kupokea taarifa ya kuwapo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani.

Taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii leo Jumamosi Oktoba 2, 2021 tangu asubuhi na kudhibitishwa na Mjumbe wa Sekretarieti, Habari na Mawasiliano wa Bawacha, Devotha Minja, zimeeleza wanawake hao wamekamatwa wakati wakifanya mazoezi katika viwanja vya Tanganyika Packres eneo la Kawe.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Kanda Maalum, Jumanne Muliro inasema watu hao walikuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani kwa kutengeneza hisia zenye mtazamo wa kisiasa. “Nimepokea taarifa ya watu waliokamatwa, walikuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani kwa kutengeneza hisia zenye mtazamo wa kisiasa kupitia kivuli cha mazoezi,” amesema Muliro.

Amesema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo, upelelezi utakapokamilika na ikibainika kilichofanyika ni viashiria vya uvunjifu wa amani, taratibu nyingine za kisheria zitafuata ikiwemo kuwafikisha mahakamani. Minja amesema wanawake hao walikamatwa wakati wanafanya mazoezi ya kukumbia na wakapelekwa kituo cha Polisi Wazo.

“Ilikuwa asubuhi wakati wanafanya mazoezi, polisi walifika wakiwa na magari mawili na kuanza kuwakamata bila utaratibu wala taarifa yoyote, wamepelekwa kituo cha polisi Wazo ingawa tunaendelea kufuatilia ili kupata idadi kamili ya waliokamatwa,” amesema Minja.

“Lengo la mazoezi haya, ni kuhamasisha wanawake kufanya mazoezi kila Jumamosi ili kuimarisha miili yao na kujilinda na maradhi mbalimbali ikiwemo Uviko 19,” amesema.

Alibainisha kuwa mazoezi hayo yameanza mwezi mmoja uliopita katika mikoa mbalimbali, wakati wakiendelea na utaratibu wa kuwahamasisha wanawake nchi nzima ili kujua umuhimu wa mazoezi, lakini hawajui ni kwa nini jeshi la polisi limekuwa likiingilia na kuwazuia kufanya mazoezi.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje John Mrema alisema, kinachofanywa na jeshi la polisi ni ukiukwaji wa taratibu na sheria kwa kuangalia watu wanaotakiwa kufanya mazoezi.

“Tumeona maeneo mengine Chama cha Mapinduzi wakifanya mazoezi ya kukimbia, hatujaona polisi wakizuia kinachoendelea ni uonevu na ukiukwaji wa haki na sharia,” amesema Mrema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live