Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi wadaiwa kuua, RPC aitaja malaria

48669 POLIS+PIC

Tue, 26 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza/Geita. Wakati polisi wakidaiwa kuhusika na kifo cha Jackson Charles (24), mkazi wa kijiji cha Nyakafuro wilayani Geita, jeshi hilo limesema kifo hicho kimesababishwa na ugonjwa wa malaria.

Jackson anadaiwa alikamatwa kwa tuhuma za kujihusisha kimapenzi na mwanafunzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema jana kuwa kifo cha Jackson kilichotokea Machi 24 kilisababishwa na malaria kali na ugonjwa wa kifafa.

“Jackson aligundulika kuwa mgonjwa akiwa mahabusu ya polisi na kukimbizwa hospitali na taarifa za kitabibu zinaonyesha licha ya kuumwa ugonjwa wa kifafa, pia alikuwa na malaria kali,” alisema Mwabulambo jana.

Hata hivyo, ndugu wa marehemu Pascal Charles amepinga akidai kifo hicho kimetokana na kipigo kutoka kwa askari kipindi walichokuwa wamemweka chini ya ulinzi kuanzia Machi 19.

Kuhusu majeraha yanayodaiwa kubainika wakati wa uchunguzi wa mwili wa marehemu, Kamanda Mwabulambo alisema yawezekana ni matokeo ya kuanguka chini kutokana na ugonjwa wa kifafa.

Ndugu, shuhuda

Charles alidai alishuhudia Jackson akiwa kituo cha polisi na hajiwezi kwa kile alichoelezwa ni kipigo alichopata kutoka kwa askari. “Nililazimika kumwona mkuu wa Kituo cha Polisi Butungwe kujua sababu za Jackson kukamatwa na kupigwa, niliambiwa eti ndugu yangu ni jeuri na amejisaidia haja kubwa bila kufuata taratibu za mahabusu,” alidai Paschal.

Alisema baada ya maelezo hayo na mengine, alirudi nyumbani kutoa taarifa, lakini aliporejea kituoni kwa mara nyingine kumjulia hali alielezwa kuwa ni mbaya na hajitambui.

Alisema ndugu yake alipelekwa Kituo cha Afya Chikobe kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita alikofariki dunia usiku wa kuamkia Machi 24.

“Tunashangaa kupewa taarifa kuwa ndugu yangu alikuwa na ugonjwa wa kifafa (lakini) kwa maisha yake yote hajawahi kuumwa kifafa,” alisema.

Akizungumzia uchunguzi wa mwili wa marehemu ulioshuhudiwa na ndugu na polisi, Paschal alisema ulikutwa na majeraha mgongoni na kichwani.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio la kukamatwa kwa Jackson, Shida Tibenda alisema mgambo na polisi waliomkamata walianza kumpiga baada ya kumfunga pingu mkononi.

“Walimkamata eneo la kuchomea CD, alipohoji sababu za kukamatwa walianza kumpiga kwa kutumia virungu vyao,” alidai Tibenda.

Wagoma kuzika maiti

Kutokana na utata wa kifo hicho, wakazi wa kijiji cha Nyakafuro walizuia mwili wa marehemu kufikishwa kijijini kuzikwa wakati tayari baba yake, Charles Sengerema alishaupokea kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita baada ya kutakiwa kufanya hivyo na polisi.

Akizungumza na Mwananchi, Sengerema alisema polisi ambao hawafahamu walimtaka achukue mwili kwa maziko na alikabidhiwa jeneza na kukodishiwa gari la kuusafirisha hadi Nyakafuro. “Nilikubali kuuchukua mwili wa mtoto wangu nikazike, lakini nilipokaribia nyumbani nilikuta kundi kubwa la wananchi wenye hasira walizuia gari wakishinikiza uchunguzi kubaini chanzo cha kifo na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria,” alisema.

“Siwezi kupingana na wana nzengo (jamii) kwa sababu ndio wenye dhamana ya kuzika licha ya ukweli kwamba mtoto ni wangu. Familia imeliacha suala hili kwa jamii iamue.”



Chanzo: mwananchi.co.tz