Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi wa ‘utakatishaji fedha’ mbaroni

91207 Pic+polisi Polisi wa ‘utakatishaji fedha’ mbaroni

Thu, 9 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Jeshi la Polisi limewatia mbaroni askari wake wawili wa kituo cha Himo wilayani Moshi kwa tuhuma za kuandaa jaribio la kumbambikia kesi ya utakatishaji fedha, mfanyabiashara Julius Mlay.

Katika tukio hilo, ambalo limekuwa gumzo ndani na nje ya mkoa wa Kilimanjaro na kwenye mitandao ya kijamii, polisi hao na watu wengine watatu, walishinikiza wapewe Sh140 milioni ili wamwachie mfanyabiashara huyo.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kituo cha Polisi Himo na kituo kikuu Moshi Mjini, askari hao walikamatwa jana kufuatia habari iliyoandikwa na Mwananchi, Januari 6, 2020.

Taarifa hizo zinadai baada ya taarifa hiyo, mkuu wa kituo cha Polisi (OCS) cha Himo alipewa maagizo ya kuwapeleka askari hao makao makuu ya Polisi Kilimanjaro ambako walikamatwa.

Polisi hao walikamatwa Januari 4 na kuandikisha maelezo yao na kisha viongozi wa polisi ngazi ya wilaya wakaingilia kati na kutaka jambo hili limalizwe kidiplomasia.

Kutokana na makubaliano hayo, polisi hao waliachiwa baada ya kurejesha Sh500,000 kati ya Sh2 milioni na Dola 100 walizompora raia huyo na kuahidi kumalizia zilizobaki mwisho wa mwezi.

Hata hivyo, taarifa zinadai viongozi wa mkoa wa polisi Kilimanjaro hawakuwa wameelezwa ukweli wa tukio hilo, hadi taarifa za tukio hilo zilipofichuliwa na Mwananchi, Januari 6.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Salum Hamduni alipoulizwa jana juu ya sakata hilo alithibitisha kukamatwa kwa askari hao na kwamba wanaendelea kuhojiwa.

“Suala hili tayari limesharipotiwa hapa kituoni na malalamiko yote tumeshayapokea na tunaendelea kuchunguza jambo hili na hao polisi wanaendelea kuhojiwa na jeshi la polisi,” alisema.

Kuhusu watuhumiwa wengine, Kamanda Hamduni alisema wengine waliohusishwa na tukio hilo bado jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro linaendelea kuwatafuta.

Taarifa nyingine zinadai watu hao watano si askari polisi bali ni wanaojihusisha na vitendo vya utapeli katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha ikiwamo kujifanya maofisa usalama wa taifa.

Mmoja wa watuhumiwa alimfuata raia huyo akimshawishi ambadilishie fedha za kigeni, Januari 2 karibu na lango kuu la kuingia Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa).

Akizungumza na Mwananchi Jumapili ya wiki iliyopita, mfanyabiashara huyo alidai siku ya tukio alifika mtu aliyewahi kuwa askari wa Kinapa kabla ya kufukuzwa kazi, akaomba ambadilishie dola 100 za Marekani.

“Huyo bwana namfahamu kwa hiyo akaniambia ana wageni wake wanataka kwenda `day trip’ (matembezi ya siku moja) na hata hela ya Tanzania ambayo anatakiwa kuweka kwenye simu,” alidai.

“Utaratibu ni kuwa huwezi kulipa cash (fedha taslimu) getini kwa hiyo akaomba nimpe Sh220,000 aniachie ile dola 100 na baada ya wageni wake kupanda na kushuka angechukua dola yake,” alisema.

Mfanyabiashara huyo alidai ghafla wakati amempa fedha hizo kwa ahadi atazirudisha na kuchukua dola zake, walitokea watu hao watano waliojitambulisha ni maofisa usalama wa Taifa.

“Walinikamata na kuniambia watu kama mimi ndio Rais (John) Magufuli anawatafuta washtakiwe kwa utakatishaji fedha. Wakasema nitakaa gerezani miaka mitano ndio nihukumiwe,”alidai.

Alidai kabla ya kuondoka eneo hilo, walifanya upekuzi katika ofisi yake na kukuta Sh2 milioni kwenye droo ambazo walizichukua na kumweleza anatakiwa kusafirishwa kwenda Dar es Salaam.

“Tukiwa njiani tunaelekea Himo na mimi niko katikati yao wakaniambia nijiongeze kwa kuwa nina tuhuma nzito. Nikawaomba wanisamehe wachukue ile Sh2 milioni waliyochukua,” alidai.

Hata hivyo, mfanyabiashara huyo alidai mmoja wao aliyedai ndio bosi alidai anawachezea na akamwambia bila Sh140 milioni, watampoteza njiani wakati wakielekea Dar es Salaam.

Baadaye walikubali kumwachia baada ya kufikia muafaka awape Sh30 milioni ambazo walikubaliana watapeana siku inayofuata ndipo mfanyabiashara huyo alipoamua kuripoti polisi.

Alikwenda mara ya kwanza katika kituo cha polisi Himo, lakini alitahadharishwa na mmoja wa askari wa hapo kuwa aende akaripoti suala hilo mjini Moshi.

Chanzo: mwananchi.co.tz