Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi mbaroni tuhuma utoroshaji wa madini

Killing Polisi mbaroni tuhuma utoroshaji wa madini

Sun, 1 Aug 2021 Chanzo: ippmedia.com

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bulyanhulu, Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga, Abdalah Kombo, alisema jana kuwa watu hao walikamatwa juzi majira ya saa sita usiku.

Alisema kuwa askari polisi na baadhi ya wachimbaji wa madini walikamatwa kwa tuhuma hizo.

“Ni kweli tukio hilo lipo, askari polisi na baadhi ya wachimbaji akiwamo meneja wa mgodi wanashikiliwa kwa kosa la kutorosha dhahabu lakini nisiwe msemaji sana, taratibu za kipolisi zinaendelea, itakapodhibitika, hatua za kisheria zitachukuliwa," alisema.

Ofisa Madini wa Mkoa wa Kahama (mkoa kisekta), Joseph Kumburu, akizungumza na Nipashe kwenye eneo la tukio, alisema watu saba wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kutorosha mawe yanayosadikiwa kuwa na dhahabu.

Alisema serikali imeingilia kati na kuuhoji uongozi wa mgodi na mawe yaliyobakia yalioshwa na kupatikana na gramu 900.

Alisema kuna uwezekano mkubwa mawe yaliyopotea yana dhahabu nyingi na ndiyo sababu wanashikiliwa ili ijulikane yalikopelekwa.

“Namba ninayojua ya watu walioshikiliwa ni saba, wamo viongozi wa mgodi akiwamo meneja. Kuhusu askari, sina taarifa hiyo.

"Lakini, askari huenda walikuwa kazini, kwa maana hiyo lazima wakisikia kelele za wizi wanakwenda," alisema.

Mwenyekiti wa Mgodi huo wa Mbaga Patinas Gold Mine, Joseph Makoba, alikiri kutokea kwa tukio hilo lakini akasita kuwahusisha moja kwa moja askari polisi katika tuhuma hizo.

“Ni kweli kwamba usiku wa kuamkia juzi majira ya saa sita, zipo tuhuma za watu kudokoa dhahabu, kuanzia hapo tulivishirikisha vyombo vya dola na tukachukua hatua stahiki kuanzia kwa viongozi wenzetu katika mgodi.

"Baadhi ya watu wamechukuliwa na vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi na tutahakikisha tunashirikiana navyo ili kubaini nani anajihusisha na tabia hiyo mbaya," alisema Makoba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, George Kyando, akizungumza na Nipashe kuhusu tuhuma za vijana kutorosha mawe hayo, alisema tukio hilo limeripotiwa kwake na amechukua hatua kadhaa.

"Nimeshamtuma RCO ili akachunguze tukio zima na baadaye kutalitolea ufafanuzi kwa vyombo vya habari.

"Kwa sasa ngoja kwanza uchunguzi ufanyike nitawapeni ufafanuzi mzuri baada ya kuletewa taarifa kamili juu ya tukio hilo kwani tayari nimemtuma RCO, naamini atafanya kazi nzuri, nanyi kupeleka ujumbe uliokamilika,” alisema Kyando.

Chanzo: ippmedia.com