Askari wa Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, Sajenti Ismael Katenya (48), anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Manyara, akidaiwa kukutwa akisafirisha bunda 340 za dawa za kulevya aina ya mirungi.
Inadaiwa kuwa Katenya alikuwa anasafirisha bunda hizo 340 zinazokadiriwa kuwa ni kilo 140 alizozifunga kwenye magunia manne akitoka Arusha akielekea mkoani Mara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi (ACP), George Katabazi akizungumza leo Januari 22, 2024 amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Kamanda Katabazi amesema askari huyo alikamatwa Januari 22, 2024 saa 9 alasiri katika Mtaa wa Silaloda Tarafa ya Endagikot wilayani Mbulu.
Amesema Polisi huyo anadaiwa alikuwa anasafirisha dawa hizo za kulevya kwenye gari aina ya Nissan Patrol station wagon.
Amedai kuwa polisi huyo alifunga dawa hizo ndani ya magunia manne ambapo kila gunia moja alipakia bunda 50, bunda 40 zilikuwa ndani ya mfuko wa salfeti, bunda 87 zilikuwa kwenye begi jeusi kubwa na bunda 53 ndani ya begi dogo jeusi.
"Alipakia dawa hizo za kulevya ndani ya gari na kusafirisha kama mizigo ndipo akakamtwa na askari waliokuwa doria," amesema Kamanda Katabazi.
Mmoja kati ya shuhuda wa tukio hilo, Abdilahi Bayo amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kumkamata bila kujali ni askari mwenzao.