Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi matatani wakidaiwa kuua

Polisisspicc Data Kijana anayedaiwa kuuawa na polisi kwa tuhuma za kuwa mhalifu, Salum Kimweri enzi za uhai wake.

Mon, 24 Jan 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Wakati mashuhuda wakisema kuwa kijana anayetajwa kwa jina la Salum Kimweri amekufa kwa kupigwa risasi baada ya vurugu iliyotokana na ugomvi wa kugombea Sh2,000 kwenye kamari, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar limekiri kuua mtu katika tukio hilo, likidai kuwa alikuwa akitafutwa kwa kutaka kupora pikipiki.

Tukio hilo lilitokea juzi eneo la Mburahati California jijini hapa, wakati vijana kadhaa walipokuwa wakicheza kamari na mmoja wao kudai kuwa amedhulumiwa fedha alizopata.

Akizungumzia kwa simu Jumamosi Januari 22, 2022 Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alikiri kuwa askari wake wamemuua kijana huyo, aliyekuwa na kesi ya kupora pikipiki huku kesi ikiwa imeshafunguliwa.

“Kwanza ni kweli amepigwa risasi na ni kweli ni mhalifu. Kuna mtu kama jana yake walitaka kumpora pikipiki. Si unajua kuna watu wanaokodi bodaboda, si ndiyo? Yupo mlalamikaji kabisa na ana kesi,” alieleza Kamanda Muliro.

Alisema siku moja kabla ya kifo chake, kijana huyo aliyepigwa risasi alikwenda kukodi pikipi akiwa na wenzake katika eneo la Magomeni Kagera.

“Yeye alidhani kuwa mwenye pikipiki hamjui, akataka kumpora, akapiga kelele watu wakamwokoa, waliotaka kumpora wakakimbia,” alisema Kamanda Muliro na kuongeza kuwa kijana huyo alitoka jela hivi karibuni baada ya kupata msamaha.

Aliongeza: “Kumbe yule waliyetaka kumpora, hawakujua kama ni mtoto wa eneo la kwao. Kwa hiyo mwenye pikipiki akawachukua polisi akawapeleka na kuwaambia yule jamaa aliyetaka kunipora yupo kule anacheza kamari na amevaa shati hili na amevaa kofia hii.”

Hata hivyo, alisema wakati Polisi wakifika eneo hilo, yule kijana aliyetakiwa kukamatwa alikimbia, lakini polisi wakafanikiwa kumrushia risasi mwenzake aliyekuwa na silaha ya moto.

“Yule mwenzake alikuwa na pistol na imekuwa seized (imekamatwa) pale, wakataka kushambulia polisi. Kwa hiyo huyo wanayesema amekufa, alipigwa risasi ya bega na akapelekwa hospitali akafariki,” alisema Muliro.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kagera Makurumla, Kimwaga Shize, ambaye aliongea kwa kifupi, alisema yeye aliona Polisi muda wa saa moja wakiwa wamesimamisha gari lao wakashusha machela na kwenda nyuma.

‘‘Lakini sikuwa na taarifa yoyote ya nini kinachoendelea mpaka nilipoona wanatoka wakiwa wamebeba mwili.

Mashuhuda watofautiana na Polisi

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, akiwemo Neema Steven walisema kulikuwa na tukio la ugomvi katika eneo ambalo vijana walikuwa wakicheza kamari nyumbani kwa mchumba wa marehemu.

Alisema ugomvi huo ulikuwa kati ya kijana aliyemtaja kwa jina moja la Kibrash na mwenzake anayeitwa Salum Kimweri.

Neema aliendelea kueleza kuwa, wakati wakiwa wanacheza kamari kuliibuka mzozo, huku mmoja akisema amekula Sh2,000 huku mwingine akisema hajala.

“Kibrash ndiye alikuwa anasema amekula Sh2,000 na kutaka apewe hela hiyo, alizidi kuongea na kusema hatakubali na kusema atarusha mawe eneo hilo na kuondoka.

“Haikupita muda akarudi hapa nyumbani na kuingia moja kwa moja kumpora kofia Salum na kukimbia nje,” alisema Neema.

Aliendelea kusimulia kuwa, shemeji yake huyo hakukubali, wakaanza kupigana na kuvutana na kofia hiyo, hadi watu walipojitokeza na kuwaamulia na ndipo Kibrash akaondoka zake.

“Baadaye Kibrash akarudi tena, akasema hatakubali na atakwenda polisi kumsingizia shemeji yake huyo kuwa amemuibia pikipiki,” alisema shuhuda huyo.

Neema alisema ilibidi ampigie dada yake anayeitwa Violet Muro ambaye ni shemeji wa Salum kumweleza kuhusu ugomvi huo na aliahidi kuilipa hiyo hela inayogombewa.

“Muda wa saa 12 jioni tukamuona tena Kibrash kaja lakini safari hii alikuwa na dada mmoja anaitwa Tedy na walikaa mbali kidogo na nyumba wakawa wanazungumza.

“Muda haukupita ndio tukaona watu wakiwa wanakimbizana huku kukiwa na polisi waliovaa kiraia na baadaye kidogo, tukapata habari kwamba Salum kafariki,” alisema Neema.

Kwa upande wake Violet Muro, ambaye ni mke wa marehemu alisema ilikuwa saa moja akiwa kwenye maombi alipigiwa simu kuelezwa ugomvi huo wa Kibrash na mume wake na kuahidi kumlipa hiyo pesa.

Lakini hakuonyesha kuridhikana, huku akimwambia ataenda kumfungulia kesi ya wizi wa bodaboda.

‘‘Pia aliahidi kwamba akiwakosa polisi, atarudi na wahuni, na wakati huo akinionyesha kisu alichokuwa amekiweka ndani ya shati,’’ alisema Violet.

Mwingine apasuliwa korodani

Wakati polisi wakiwatawanya watu katika eneo hilo kwa risasi, mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Musa Kisoma (32) mkazi wa Tandale, alidai kujeruhiwa akiwa anapita njia kutoka kwenye mihangaiko yake.

Akizungumza akiwa amelazwa katika hospitali ya Mwananyamala, alisema alikuwa akipita katika Mtaa wa Mburahati California na kukutana na kundi la watu likiwa linakimbizwa na polisi waliokuwa wakifyatua risasi juu.

Baada ya kuona vile naye akajihami kukimbia, ndipo akasikia maumivu sehemu za siri na kushindwa kutembea.

“Ilibidi nimpigie simu rafiki yangu Ally Mayanga kumtaarifu kwamba nimepigwa risasi na kumuomba aje anichukue kunipeleka hospitali na baada ya hapo sikujua tena nini kinaendelea mpaka niliposhtuka na kukuta nipo hospitali,” alisema huku akieleza wasiwasi wake kama ataweza kumtungisha mimba mwanamke, kwa kuwa mara kwa mara madaktari wamekuwa wakimuuliza kuhusu idadi ya watoto alionao.

Aliwataka polisi kuwa makini wanapofanya misako ya kuwatafuta wahalifu, kwani wamekuwa wakigharimu maisha ya watu wasio na hatia.

Daktari azungumza

Mwananchi lilipofika hospitalini hapo wodi namba tano, alipolazwa majeruhi, mwandishi alimsikia daktari aliyekuwa akimhudumia akiwaelezea ndugu wa majeruhi kwamba, ndugu yao wamemkuta katobolewa korodani.

Hata hivyo, alisema wamempatia matibabu kwa kumshona lakini wanampa rufaa ya kwenda hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya kuchunguzwa zaidi mfumo wa mkojo.

Jingine alisema kinachowapa wasiwasi ni kuona tundu ilipoingia kitu wanachodhani ni risasi lakini hawaoni ilipotokea.

“Unajua risasi ikiingia sehemu lazima kuwe na mahali imetokea, sasa kwa huyu ndugu yenu hatulioni hilo, jambo linalotupa maswali zaidi imetokea wapi, huenda katika vipimo zaidi wenzetu Muhimbili wakalitambua hilo,” alieleza daktari huyo huyo.

Naye Mayanga, alisema alimkuta rafiki yake katika hali mbaya ya kujeruhiwa na kumkimbiza hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Hata hivyo, alisema wakati wanamvua nguo alishuhudia nyamanyama zikiwa zimemwagika kwenye nguo yake ya ndani na suruali na kwa kuwa ilikuwa inambana walimvua kwa kuikata na kisha kuitupa kwenye ndoo ya kutupa uchafu iliyopo hospitalini hapo. Mayanga alisema tayari alitolea maelezo tukio hilo kituo cha Polisi Mburahati wa ajili ya taratibu za kupata PF3.

Soma zaidi:Watano wa familia moja wauawa mkoani Dodoma

Chanzo: www.mwananchi.co.tz