Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi kuwapima ulevi madereva wanaotoka baa

12389 Pic+ulevi TanzaniaWeb

Fri, 17 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linakusudia kuanzisha kampeni dhidi ya madereva walevi kwa kutega maeneo ya karibu na baa na kuwapima madereva wote wanaotoka kwenye maeneo hayo ya starehe kubaini kiwango cha kilevi walichokunywa.

Akizungumza jana Agosti 16, 2018 wakati wa mafunzo maalum kwa madereva waliopata leseni bila kupitia mafunzo ya udereva, mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Mwanza, Mkadam Mkadam alisema mpango huo unalenga kuhakikisha hakuna dereva aliyelewa anayeendesha gari.

“Ulevi ni miongoni mwa sababu za ajali nyingi za barabarani; tutaanza kuwapima madereva wote wanaotoka baa kubaini kiwango cha pombe walichokunywa. Nimesema hili hadharani ili kuwapa tahadhari wenye tabia ya kuendesha gari wakiwa wamelewa,” amesema Mkadam.

Amewataka washiriki zaidi ya 400 wanaohudhuria mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Chama cha Shule za binafsi za Udereva Tanzania (Chashubuta), kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima zinazoangamiza maisha ya watu wasio na hatia.

Kwa upande wake, mkufunzi kutoka Chashubuta, Sabian Dominic amesema chama hicho kimeandaa mafunzo hayo ili pamoja na kuwakumbusha madereva hao sheria, kanuni, taratibu na wajibu wao wawapo barabarani, lakini pia waweze kupata sifa za kumiliki leseni za udereva.

Mwenyekiti wa Chashubuta, Majid Igangula alisema mafunzo hayo yatakuwa endelevu hadi madereva wote waliopata leseni bila kuhudhuria mafunzo wafikiwe.

Chanzo: mwananchi.co.tz