Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi kumpa dhamana kiongozi wa Chadema

58689 Pic+chadema

Mon, 20 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mara. Katibu wa Chadema kata ya Nyarero Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara,  Matibwi Magoiga anayeshikiliwa na polisi  tangu Mei 15, 2019 anatarajiwa kuachiwa kwa dhamana leo Jumatatu Mei 20, 2019.

Magoiga anashikiliwa kwa tuhuma za kuchochea mapigano ya kikabila.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi  Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe amesema Magoiga ataendelea kuwa chini ya uangalizi wa polisi kwa uchunguzi.

“Nimeagiza aachiwe kwa dhamana  ninaamini amri yangu itatekelezwa wakati wowote leo. Lakini tutaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tuhuma zinazomkabili kubaini kama ni za kweli au uongo,” amesema Kamanda Mwaibambe.

Amesema pamoja na kuchunguza tuhuma hizo zikiwemo za kuhusika na mapigano ya koo, polisi pia inachunguza malalamiko ya mtuhumiwa huyo kwamba madai dhidi yake ni ya kutungwa na watu wenye hila.

“Polisi hatubambikii watu kesi. Tukipata taarifa zozote za uhalifu tunazifanyia kazi na ikibidi tunamtia mbaroni mtuhumiwa kukamilisha upelelezi. Huyu (Magoiga) katueleza mambo mengi ikiwemo madai ya kuundiwa tuhuma kwa hila, tunayachunguza na tutachukua hatua,” amesema.

Habari zinazohusiana na hii

Akizungumzia kitendo cha jeshi hilo kumshikilia mtuhumiwa huyo kwa siku kadhaa bila kuwajulisha familia na ndugu huku ikikana kujua alipo, Kamanda Mwaibamba amesema waliokuwa wakimtafuta mtuhumiwa huyo hawakutumia njia sahihi kumtafuta na kujua ukweli zaidi ya kuzusha madai ya kutekwa.

"Askari walikwenda na kumchukua nyumbani kwake yeye pamoja na wenzake watatu. Kwa sababu za kiupelelezi tuliwahifadhi katika mahabusu ya vituo tofauti vya polisi,” amefafanua Kamanda huyo.

Pamoja na Magoiga, Watu wengine waliokamatwa na polisi usiku wa kuamkia Mei 15, 2019 ni Mwita Mgesi, Charles Magige na Inchota Mchuma ambao tofauti na Magoiga, wao walipatikana siku ya pili wakiwa katika kituo cha Polisi Borega.

Katibu wa Chadema Jimbo la Tarime Vijijini, Sunday Magacha na Mrimi Zablon ambaye ni katibu wa mbunge wa Tarime vijijini, John Heche wameieleza Mwananchi kuwa  Mei 19, 2019 familia na ndugu na viongozi wa Chadema wilayani humo walimtafuta Magoiga katika vituo vyote vya polisi bila mafanikio.

Chanzo: mwananchi.co.tz