Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi hawakumwelewa Rais Magufuli aliposema Watanzania si wajinga?

69658 Pic+polisi

Sun, 4 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwandishi wa habari, Erick Kabendera alikamatwa na jeshi la polisi hivi karibuni. Namna alivyokamatwa ilileta shida kwa wananchi kuelewa kama alikamatwa na alikuwa kwenye mikono salama ya dola au alitekwa?

Ndugu, marafiki na jamaa waliingia kazini kumtafuta. Taarifa zinasema Kabendera hakupata nafasi ya kuwajulisha watu wake muhimu, akiwemo mwanasheria wake kuhusu kukamatwa kwake. Inaelezwa simu yake ilipoteza mtandao (network) ghafla.

Tangu alipokamatwa ndugu, marafiki na jamaa mbalimbali, wakiwemo wanaharakati walianza kubisha hodi katika vituo mbalimbali vya polisi.

Polisi Oysterbay, Kinondoni hakuwapo, Kituo Kikuu Dar es Salaam (Central) hakupatikana, Mburahati (kituo kipya kikubwa Dar) nako hakuonekana. Polisi Makao Makuu hawakuwa naye. Maeneo yote hayo, jina la Kabendera liliitwa mahabusu pasipo kuitikiwa.

Taarifa za upande wa ndugu na marafiki wa Kabendera, zilieleza kuwa maofisa waliosema ni polisi walikwenda nyumbani kwa Kabendera, Mbweni, Dar es Salaam na kumkamata.

Swali ambalo liligonga vichwa vya watu ni kwa nini polisi hawakutaka kukiri mapema kuwa wanamshikilia na kutaja kituo cha polisi alichopo?

Pia Soma

Siku ya pili jioni Kamishna wa Polisi, Kanda Maalumu, Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ndipo alikiri kuwa Kabendera anashikiliwa na polisi kutokana na utata wa uraia.

Mambosasa alisema, Kabendera alipewa wito wa polisi lakini aliupuuza ndio maana alifuatwa na kukamatwa.

Hilo la kuitwa na kupuuzia wito, mwenye nafasi ya kulijibu ni Kabendera mwenyewe au wakili wake. Hata hivyo, pamoja na Mambosasa kukiri polisi kumshikilia lakini hakutaja kituo alichopo.

Ofisi ya Mambosasa ipo Central, Barabara ya Sokoine, mkabala na Stesheni, Dar. Ndugu walikwenda Central kwa mara nyingine lakini hawakupata majibu ya alipo Kabendera, maana hakuwamo kwenye mahabusu za kituo hicho.

Siku ya tatu asubuhi, ndugu na marafiki walifanikiwa kumwona Kabendera, Kituo cha Polisi Kilwa Road. Angalau kuanzia hapo, utulivu wa awali ukawepo, maana ilithibitika kwamba alikuwepo kwenye mikono ya polisi.

Baada ya hapo, wasiwasi lazima uendelee katika maeneo mawili; la kwanza ni kwa nini polisi hawakuwa na lugha iliyonyooka kuhusu kumkamata na mahali walipomshikilia? Mbona ndugu na wakili wake hawakupashwa habari mapema?

Wasiwasi wa pili ni kwa nini polisi walipitisha saa 48 wakimshikilia Kabendera bila kumfikisha mahakamani mpaka watetezi wa haki za binadamu walipopeleka maombi mahakamani kutaka mahakama iliamuru Jeshi la Polisi kumpeleka mahakamani?

Tukubali kuwa polisi waliingia kwenye kesi ya uhamiaji kumhusu Kabendera kwa sababu waliombwa na Idara ya Uhamiaji. Swali; suala la utata wa uraia wa Kabendera lina unyeti gani mpaka kutumia nguvu kubwa ya kumkamata na kumficha kwa zaidi ya saa 24 bila familia yake kujua?

Kabendera ana wazazi wake hapa Tanzania. Inaelezwa mama yake ni mgonjwa, lakini baba yake yupo sawa. Kwa nini Erick ahojiwe uraia wakati yeye ni mzaliwa, wazazi wake wapo hawajafuatwa kuhojiwa? Polisi na Uhamiaji wangefupisha mzunguko kwa kuwahoji wazazi kuliko yeye.

Je, walifanya makusudi kutowahoji wazazi wa Kabendera na kumhoji moja kwa moja au bahati mbaya? Vipi, uraia wa wazazi hauna shaka lakini wa mtoto wao ndio una utata? Au wameshathibitisha kuwa wazazi wa Kabendera si raia, kwa hiyo wanajiridhisha kupitia mtoto wao?

Polisi wamwelewe JPM

Kwa namna ambavyo polisi wamelishughulikia suala la Kabendera, imetengeneza maswali mengi tata. Zaidi, Watanzania wanajiuliza kilichopo nyuma ya kukamatwa kwake. Wanahisi kulikuwa na zaidi ya hiyo kesi ya uraia.

Novemba mwaka jana, alitekwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘MO’. Mazingira ya kutekwa kwake na mpaka alipoachiwa yaligubikwa utata. Maswali yalikuwa mengi na polisi hawakujishughulisha kuyajibu. Rais John Magufuli, aliwaambia polisi kuwa Watanzania si wajinga!

Inaonekana polisi hawakumwelewa vizuri Rais Magufuli. Wanapaswa kutambua kuwa alichowaambia ni kwamba wanapofanya kazi zao wahakikishe hawaachi maswali, kwani Watanzania wana uelewa wa kutosha. Palipo na utata wanajua hata kama watanyamaza.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Simon Kanguye ana mwaka wa pili, tangu alipochukuliwa na watu waliojifanya ni maofisa kutoka vyombo vya usalama Julai 2017. ‘Maofisa’ hao walikwenda nyumbani kwa Kanguye, wakamtwaa na kuondoka naye. Mpaka leo hajulikani alipo, kama yu hai au la.

Mwandishi Azory Gwanda, alitekwa na watu ambao hawakufahamika wakaenda naye mpaka shamba kumfuata mkewe, akachukua ufunguo wa nyumbani, hakupata mwanya wa kumwambia aliokuwa nao ni akina nani. Ni mwaka mmoja na miezi tisa sasa tangu Azory atoweke.

Mwanamuziki Roma Mkatoliki na wenzake watatu, walitekwa Oysterbay, Dar na watu waliokuwa na bunduki pamoja na pingu, wakijionesha ni askari. Siku tatu baadaye waliachiwa na kutelekezwa ufukwe wa Bahari ya Hindi, Ununio, wakiwa wamepigwa na kuumizwa, wamevunjwa meno na kadhalika.

Polisi wanatakiwa kufahamu kuwa watekaji wamekuwa wakijifananisha na polisi ili kufanikisha malengo yao. Sasa basi, kitendo cha polisi kumkamata Kabendera na kuchelewa kueleza ukweli, kilisababisha wananchi wajiulize maswali mengi. Maswali hayo si mazuri kwa taswira ya Jeshi la Polisi.

Polisi wafanye kazi zao kwa weledi, hivyo ndivyo kuwaheshimu Watanzania. Kufanya kinyume chake ni kuwafanya wananchi wajinga, kitu ambacho Rais Magufuli alishawaonya.

Chanzo: mwananchi.co.tz