Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi aeleza watuhumiwa walivyodakwa kesi dawa za kulevya

Hukumu Pc Data Polisi aeleza watuhumiwa walivyodakwa kesi dawa za kulevya

Sat, 25 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dar es Salaam. Shahidi Raphael Ngongi katika kesi inayomkabili Justine Kayombo na mkewe Veronica Emmanuel, ameielezea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jinsi alivyowakamata washtakiwa hao wakiwa na dawa zinazodaiwa kuwa ni za kulevya.

Ngongi ambaye ni Ofisa wa Polisi kutoka Ofisi ya Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam amesema aliwakamata washtakiwa wakiwa na vifurushi wiwili vya majani ya bangi, kete mbili za bangi pamoja na vifurushi vitatu vya heroin vilivyofungwa kwenye mfuko wa nailoni.

Ofisa huyo ameyasema hayo leo Ijumaa, Novemba 24, 2023 wakati akitoa ushahidi wake katika kesi ambayo Kayombo na mkewe wanakabiliwa na mashtaka ya kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa gramu 1.18 na heroin zenye uzito wa gramu 9.48.

Shahidi huyo akiongozwa na Wakili wa Serikali Winia Samson, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Evodia Kyaruzi alidai Februari 3, 2020; yeye pamoja askari polisi wenzake, wakiwa kwenye doria eneo la Kimara Michungwani, walipewa taarifa na msiri kuwa mshtakiwa Kayombo anajihusisha na dawa za kulevya.

"Msiri alituonyesha nyumba anayoishi Kayombo, nikiwa na askari wenzangu tulikwenda kugonga kwenye mlango wake na alitoka pamoja na Veronica, tukajitambulisha ni askari polisi tunataka kufanya upekuzi," alidai Ngongi.

Baada ya kujitambulisha, walimtafuta mjumbe wa eneo hilo ambaye alishuhudia wakati wanafanya upekuzi katika chumba cha washtakiwa hao.

Ngongi alidai walifanya upekuzi na kukuta vifurushi viwili vya majani ya bangi na kete mbili za bangi, vifurushi vitatu vya unga wa dawa za kulevya uliofungwa kwenye nailoni pamoja na ‘kisosi’ cha udongo kilichokuwa na vipisi vya sigara pamoja na mfuko ya nylon inayotumika kufungia dawa hizo.

Kisha akawaeleza askari wenzake wajaze vielelezo hivyo kwenye fomu ya ukamataji ya kutoka Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA)

Baada ya kujaza vielelezo hivyo kwenye fomu hiyo washtakiwa walikamatwa na kupelekwa Polisi kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

Shauri hilo limeahirishwa hadi Novemba 28, 2023 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi

Katika kesi ya msingi kati ya Februari 3, 2020 eneo la Kimara Michungwani washtakiwa hao walikamatwa wakiwa na dawa za kulevya gramu 1.18 aina ya bangi pamoja heroin gramu 9.48.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live