Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi adaiwa kuua kwa risasi

629961e5553bc38f54f7ca1a9072341a.png Polisi adaiwa kuua kwa risasi

Mon, 26 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

POLISI wa Kituo Kikuu cha Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, anadaiwa kumpiga risasi raia aliyetambuliwa kwa jina la Yohana Nasieli katika mazingira yanayohusishwa na mapenzi. Majirani na ndugu wa marehemu wanadai kuwa, tukio hilo lilitokea Aprili 12 mwaka huu saa 1.35 usiku katika Mtaa wa Sabasaba, Kata ya Monduli Tarafa ya Kisongo wilayani humo.

Inadaiwa kuwa siku ya tukio, Nasieli alikuwa na ugomvi na mkewe, Paulina Kiliani (37), akimtuhumu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na polisi aliyedaiwa kuua (jina linahifadhiwa).

Kwa mujibu wa vyanzo, siku ya tukio Nasieli aligombana na mkewe hadi wakapigana na ndipo Paulina akampigia simu ya kiganjani polisi huyo kumpa taarifa kuwa amepigwa na mumewe.

Alielezwa kuwa, baada ya kupata taarifa hizo, askari huyo na mwenzake wakiwa na silaha walikwenda eneo la tukio. Inadaiwa kuwa baada ya Nasieli kumwona polisi anayemtuhumu kuwa na uhusiano na mkewe, alizidi kukasirika na kuongea kwa jazba kisha akaingia ndani kuchukua panga kwa lengo la kumdhuru askari polisi huyo.

Vyanzo vya habari vinadai kuwa kabla ya Nasieli kutimiza lengo lake, askari polisi huyo alimpiga risasi kifuani upande wa kushoto na mguuni na Nasieli akafa papo hapo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema Nasieli alijeruhiwa kwa risasi mguu wa kushoto na kwenye bega la mkono wa kushoto.

Taarifa ya Kamanda Masejo ilieleza kuwa, raia huyo alikaidi amri ya polisi ya kutaka kumkamata na alitaka kumkata askari kwa panga alilokuwa nalo mkononi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Paulina ni mfanyabiashara na anaishi eneo la Sabasaba. Kamanda Masejo alieleza kuwa, awali mama huyo alifika Kituo cha Polisi akamtambulisha Nasieli kuwa ni mpenzi wake na kufungua kesi dhidi ya Nasieli ya kutolewa lugha ya matusi.

Alieleza kuwa, mchana wa siku ya tukio, mlalamikaji alirudi tena katika kituo cha Polisi akidai kuwa mpenzi wake alimpiga na kumsababishia majeraha kwenye kidole na sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kamanda Masejo alieleza kuwa, Nasieli pia aliwafungia wanawe na mtoto wa jirani ndani ya nyumba kwa nia ya na kuwadhuru na baada ya Polisi kupata taarifa walikwenda eneo la tukio kwa nia ya kuwaokoa watoto na kumkamata mtuhumiwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya kufika eneo la tukio waligonga mlango uliokuwa umefungwa na wakati wanaokoa watoto, walimuona Nasieli akiwa amejificha akiwa na panga mkononi na akafuata askari kwa lengo la kuwadhuru.

Alieleza askari hao walimuamuru Nasieli asimame, lakini hakutii na aliendelea kuwafuata akiwa amenyanyua panga. Kwa mujibu wa kamanda huyo, askari hao walirudi nyuma mitaa kadhaa, lakini Nasieli aliendelea kuwafuata na askari walianza kukimbia, wakapotezana na mtuhumiwa akawa anamfukuza askari polisi mmoja.

Alisema askari polisi aliyekuwa akikimbizwa alipiga risasi mbili juu ili mtuhumiwa asimame, lakini alizidi kumfuata hivyo akampiga risasi mguu wa kushoto, lakini Nasieli alizidi kumsogelea askari ambaye kwa wakati huo alikuwa ameanguka.

Kiongozi huyo wa polisi alisema Nasieli alimfikia askari polisi na alitaka kumnyang’anya silaha aina ya SMG. Kamanda Masejo alieleza kuwa katika purukushani hiyo, polisi alimpiga risasi Nasieli kwenye bega la kushoto akavuja damu nyingi.

Kwa mujibu wa Polisi, Nasieli aliaga dunia wakati akipata tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Monduli.

Chanzo: www.habarileo.co.tz