Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi, TEC waonya vurugu

Waonya Pic Data Polisi, TEC waonya vurugu

Sun, 26 Dec 2021 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Wakati Watanzania wakiendelea kutakiana heri ya Sikukuu ya Krismasi ambayo ni leo, tahadhari mbalimbali zimeendelea kutolewa na Jeshi la Polisi ili kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Wakati huohuo, Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki (TEC), nalo limewaasa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidin ya ugonjwa wa Uviko-19.

Tahadhari za Jeshi la Polisi

Jijini Arusha, Jeshi la Polisi mkoani humo limewataka wakazi wake kuchukua tahadhari za uhalifu na kutopeleka watoto wadogo kwenye majumba ya vileo wakati wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justin Masejo alisema kuelekea sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya, jeshi hilo limejipanga kuhakikisha kunakuwa na usalama maeneo yote.

“Katika mkesha wa Mwaka Mpya tumeimarisha doria za askari wa miguu na magari, lakini tunaomba wananchi pia kuchukua tahadhari kwa kutowapeleka watoto maeneo ya vilevi na madereva kuacha kuendesha magari wakiwa wamelewa” alisema.

Advertisement Mkoani Manyara, Jeshi la Polisi limewataka wananchi waweke ulinzi majumbani kujilinda wakati huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, japokuwa nao watakuwa wanalinda usalama wao na mali zao.

Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Kamishna Msaidizi (ACP) Benjamin Kuzaga, alisema hayo jana wakati akielezea mikakati ya ulinzi wa polisi kwenye sikukuu za mwisho wa mwaka, kwamba pamoja na polisi kuimarisha ulinzi, raia pia wajitahidi kuwa walinzi wa mali zao.

Alisema jukumu la ulinzi wa raia na mali zake siyo la polisi pekee, bali jamii kwa ujumla hivyo wananchi nao wahakikishe wanaimarisha ulinzi.

Aliwataka kutokaribisha ovyo watu majumbani ambao ni wageni wasiowafahamu, kwani wengine ndiyo wanaogeuka kuwa wezi wa majumbani.

“Jeshi la Polisi tumejipanga kuhakikisha tunawachukulia hatua kali wale wote watakaokuwa wanatumia kwa uzembe vyombo vya moto wakiwa wamelewa,” alisema.

Mkoani Dar es Salaam, jeshi hilo tayari limeshapiga marufuku matumizi ya milipuko ya baruti na fataki katika kipindi chote cha sikukuu za Krismasi na mkesha wa mwaka mpya.

Pia limepiga marufuku watoto wadogo kushiriki katika nyumba za starehe na muziki maarufu kama disko toto na uchomaji moto matairi.

Jijini Dodoma kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Onesmo Lyanga alisema walinzi 600 wamepangwa kulinda usalama kwa wakazi wa jiji hilo na vitongoji vyake, huku polisi wakipiga marufuku disko toto katika kipindi cha sikukuu.

Alisema idadi ya walinzi inajumuisha polisi, askari wengine na wananchi wa kawaida ambao wameshaelekezwa nini cha kufanya katika kipindi cha sikukuu.

Lyanga alisema ulinzi huo utahusisha askari wa miguu, farasi, mbwa, magari, pikipiki na vyombo vingine watakavyoona vinafaa katika kusaidia usalama.

Huko Njombe. Jeshi limewataka wazazi na walezi kuacha kuwalaza watoto wao chumba kimoja na watu wazima katika msimu huu wa sikukuu, ili kuwaepusha kufanyiwa ukatili.

Salamu za TEC na KKKT

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limewataka waumini wake pamoja na Watanzania wote kwa ujumla kusheherekea sikukuu hiyo, kwa kuendelea kudumisha amani huku likiwakumbusha kuwasaidia wenye uhitaji maalumu.

Hayo yalisemwa na Naibu Katibu wa baraza hilo, Padri Chesco Msaga alipozungumza na Mwananchi jana na kuwataka waumini kusheherekea kwa upendo na utulivu.

“Katika sikukuu hizi tungependa amani iendelee kudumu kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa kwa ujumla, pia Wasisheherekee wakajifurahisha wenyewe, wawakumbuke wajane, yatima, wagonjwa na wote wenye uhitaji,”alisema.

Vilevile aliwataka watu wote kuendelea kujikinga na ugonjwa wa Uviko-19 kwa kuchukua tahadhari zinazoshauriwa na wataalamu wa afya ikiwamo uvaaji wa barakoa pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.

“Ugonjwa wa Uviko-19 bado upo hivyo tuendelee kuchukua tahadhari hata tunavyoingia katika nyumba za ibada, Sikukuu hizi zisiwe chanzo cha ugonjwa huo kusambaa zaidi,”alisema.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Fredrick Shoo ameomba Mungu awape Watanzania macho ya kuwaona na mioyo ya huruma wote wanaoteseka na kulia kipindi hiki cha sikukuu.

“Tunapoadhimisha sikukuu ya mwaka huu, twapaswa kufurahi na kumshukuru Mungu kwa upendo wake mkuu kwetu sisi wanadamu. Tusifurahi tu peke yetu, bali tuwakumbuke wenzetu walio na huzuni na majonzi kwa sababu mbalimbali” alisema.

Imeandikwa na Mariam Mbwana, Joseph Lyimo, Mussa Juma, Habel Chidawali na Seif Jumanne.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz