Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi Pwani waua majambazi 3

737a77d389d2889480a182b423113670 Polisi Pwani waua majambazi 3

Mon, 24 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WATU watatu kati ya kumi waliovamia kiwanda cha Samaki Investment kilichopo Zinga wilayani Bagamoyo wamepigwa risasi na Polisi na kufa.

Hayo yalisemwa na Kamanda wa Polisi mkoani humo, Wankyo Nyigesa jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Nyigesa alisema majambazi hao waliuawa jana saa 8 usiku kwenye kiwanda hicho kinachozalisha vifungashio vya kuhifadhia mazao na mifuko ya kubebea bidhaa maarufu kwa jina la sulphates.

“Mbali ya watuhumiwa hao wa ujambazi kuuawa pia tumefanikiwa kukamata silaha yao moja, gari na pikipiki ambayo walitumia wakati wa kutekeleza tukio hilo ambalo hata hivyo halikuweza kufanikiwa baada ya Polisi kuwahi kufika kwenye la tukio,”alisema Kamanda Nyigesa.

Alisema watu hao walifika kiwandani hapo kwa kutumia gari namba T 825 CVB aina ya Toyota RAV 4 rangi ya bluu na pikipiki yenye namba za usajili MC 540 BWA aina ya Haojue.

“Majambazi hao wakiwa kiwandani walianza kutoboa ukuta uliojengwa kuzunguka kiwanda hicho kwa lengo la kupata mwanya wa kuingia ndani wakiwa katika harakati hizo Jeshi la Polisi lilipata taarifa na kufika haraka kwenye tukio hilo,”alisema Kamanda Nyigesa.

Alisema Polisi walipofika ghafla walishambuliwa na wao wakajibu mapigo. “Katika upekuzi eneo la tukio na ndani ya gari la watuhumiwa kulikamatwa silaha hiyo ambayo ilikuwa haina namba, risasi tatu nzima za shot gun hiyo na maganda mawili waliyotumia kuwatisha askari Polisi na walinzi wa kiwanda hicho, mikasi mikubwa ya kukatia vyuma, kamba za kufungia mizigo aina ya kudu na mapanga mawili,”alisema Kamanda Nyigesa.

Alisema, wanaendelea na operesheni kukamata watuhumiwa wengine sita ambao wamepata majeraha madogo madogo ya risasi katika tukio hilo.

Alitoa wito kwa wananchi watakaopata taarifa au kuona watu wenye majeraha ya risasi watoe taarifa kituo chochote cha Polisi na watu waliopotelewa na ndugu zao walitamiwa kwenda hospitali ya Bagamoyo kutambua miili ya marehemu.

Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Xidowei Yu amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuwahi kufika kwenye tukio na kuokoa maisha yao na mali.

Chanzo: habarileo.co.tz