Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi Mara yaanika matukio ya uhalifu mwaka 2023

Polisi Mara Polisi Mara yaanika matukio ya uhalifu mwaka 2023

Tue, 19 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Watu 2,990 wamekamatwa na polisi mkoani Mara wakituhumiwa kwa uhalifu, yakiwamo matukio mawili ya mauaji katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2023.

Polisi pia imekusanya zaidi ya Sh812 milioni katika kipindi hicho zikiwa ni fedha za faini kutokana na makosa ya usalama barabarani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salum Morcase ametoa takwimu hizo leo, Jumanne Desemba 19, 2023 wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi ya mwaka huu.

Amesema watuhumiwa 2,170 wamefikishwa mahakamani na kati yao 1,924 wamepatikana na hatia na kupewa adhabu mbalimbali zikiwamo faini na vifungo.

"Haya yametokana na misako na operesheni tulizofanya, kubwa zaidi ni ushirikiano kutoka kwa wananchi,” amesema.

Kuhusu usalama barabarani, amesema wameshughulikia makosa 29,616 yaliyowezesha zaidi ya Sh812 milioni kukusanywa.

Amesema miongoni mwa waliokamatwa wanatuhumiwa kwa makosa ya kupatikana na dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi.

Kamanda Morcase amesema katika kipindi hicho, wamekamata mirungi yenye uzito wa zaidi ya kilo 359, bangi yenye uzito wa zaidi ya kilo 237 na pombe haramu aina ya gongo lita 6,734.

"Kwa upande wa nyara za Serikali tuliwakamata watuhumiwa wanane wakiwa na vipande 16 vya meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya Sh308.4 milioni,” amesema.

Amesema watuhumiwa wengine 46 wamekamatwa wakiwa na vipande 1,234 vya nyamapori.

Katika kipindi hicho, amesema yapo matukio makubwa matatu yaliyotokea mkoani Mara, likiwamo la Mei, lililohusisha mauaji ya madereva wa pikipiki maarufu bodaboda wanne lililotokea katika vijiji vya Nyakiswa na Nyamikoma wilayani Butiama.

Amesema tukio jingine ni la mauaji ya mkazi wa Kijiji cha Nyankanga aliyekuwa akimiliki eneo la uchimbaji madini ujenzi.

“Watuhumiwa tisa wa matukio hayo mawili wamekamatwa wakiwa na bastola iliyotumika. Wote wamefikishwa mahakamani kwa hatua zaidi," amesema.

Kamanda Morcase amesema tukio la tatu ni la kuzama kwa mitumbwi miwili ndani ya Ziwa Victoria katika Kijiji cha Mchigondo.

Katika tukio hilo watoto 14 waliokuwa wakitoka kwenye ibada walifariki dunia. Kati ya hao, 13 walikuwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Bulomba, wilayani Bunda.

Chanzo: Mwanaspoti