Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi Kilimanjaro yakamata magari yaliyoibwa

87364 Pic+polisi Polisi Kilimanjaro yakamata magari yaliyoibwa

Fri, 6 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Jeshi la Polisi mkoa Kilimanjaro nchini Tanzania, limekamata mtandao unaodaiwa kujihusisha na wizi wa magari na kufanikiwa kukamata magari manne kati ya saba aina ya Toyota Noah, yanayodaiwa kuibwa katika wilaya za Hai, Moshi na Rombo.

Wimbi la wizi wa magari aina ya Toyota Noah liliutikisa mkoa huo kuanzia Februari, 2019 ambapo magari saba yaliripotiwa kuibwa kwa wezi kuiba magari hayo yakiwa ndani ya uzio wa nyumba bila wenye nyumba kushtuka.

Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Salum Hamduni amewaambia waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 6,2019, kuwa kukamatwa kwa mtandao huo kulitokana na kukamatwa kwa mtu anayedaiwa kuwa kinara wa wizi wa magari hayo.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo,  baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo mkazi wa mji mdogo wa Himo, anadaiwa kuwataja washirika wake wengine 12 ambao bado wanaendelea kushikiliwa kwa mahojiano na wapelelezi.

Ametaja magari ambayo yaliibwa katika wilaya hizo na kukamatwa katika operesheni ya Jeshi hilo ni yenye namba za usajili T104 DDG, T706 DEE, T983 DGJ na T409 DDF ambayo wamiliki waliyatolea taarifa polisi kuwa yameibwa.

Halikadhalika katika msako huo, polisi walieleza kufanikiwa kukamata magari mengine manne aina ya Toyota IST, Toyota RAV4, Toyota Noah na Toyota Vitz ambayo wanayashuku kuwa ni ya wizi na uchunguzi kuthibitisha suala hilo unaendelea.

Chanzo: mwananchi.co.tz