Mwanga. Polisi mkoani Kilimanjaro limekamata ndoo 60 zenye ujazo wa lita 20 za samaki wachanga waliovuliwa kwa nyavu haramu (makokoro) katika bwawa la Nyumba ya Mungu wilayani Mwanga.
Akizungumzia kukamatwa kwa samaki hao, Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Hamis Issah amesema wanamshikilia Godlizen Mfinanga(37) mkazi wa kwa Mromboo jijini Arusha ambaye ndio kinara wa kuvua samaki hao haramu pamoja na Mwidin Suleiman mkazi wa Kisongo.
Aidha Kamanda Issah amesema watuhumiwa hao wamekamatwa majira ya saa 3:30 usiku jana Jumatatu kata ya Kirwa tarafa ya Lembeni wilayani humo.
"Jeshi la polisi tunawashikilia watu wawili waliokuwa wakisafirisha samaki waliovuliwa kwa nyavu haramu katika bwawa la nyumba ya Mungu majira ya saa 3:30 usiku waliokuwa wakipelekwa jijini Arusha," amesema Kamanda
Kamanda Issah amesema watuhumiwa hao watapelekwa kituo cha polisi Moshi Mjini huku taratibu nyingine za kufikishwa mahakamani zikiendelea.
Naye Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema mvuvi huyo amekua akiwasumbua kwa muda mrefu kwani alikua akiisababishia wilaya hiyo kupata hasara kwa miaka mingi.
Pia Soma
- Tanesco watua Njombe kutekeleza agizo la Rais Magufuli
- Tanzania yaiahidi Marekani mazingira bora ya uwekezaji
- VIDEO: Majeruhi 17 wa ajali ya treni waruhusiwa, watatu hali zao bado
- VIDEO: Waziri wa uwekezaji ateta na wanawake kuhusu bajeti
"Wilaya ya mwanga ingetakiwa iwe juu katika ukusanyaji wa mapato yake lakini huyo tuliyemkamata leo ametusababishia hasara kubwa sana.”
“Hii wilaya ingekuwa na uwezo wa kukusanya mapato Sh10 bilioni kwa mwaka kama kungekuwa na uvuvi halali lakini sasa hivi tunakusanya Sh20 milioni kutokana na uvuvi haramu unaoendelea," amesema Mghwira.