Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi Kagera yadai kuua watuhumiwa watatu wa ujambazi

Wed, 20 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Muleba. Jeshi la polisi mkoani Kagera limewaua watu watatu wanaosadikiwa kuwa majambazi katika pori la Ngazi Saba kata ya Nyakahura wilayani Biharamulo mkoani Kagera baada ya majambazi hao kuwashambulia polisi wakati ikisakwa bunduki aina ya AK 47 iliyokuwa imefichwa katika bonde la pori hilo.

Kamanda wa polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi ameiambia Mwananchi leo Jumanne Machi 19, 2019 kuwa watu hao walipoteza maisha juzi Jumapili na walikuwa wakitafutwa na polisi kwa muda mrefu wakihusika kufanya matukio ya utekaji magari na unyang'anyi katika maeneo ya Biharamulo, Kibondo, Kakonko na Runzewe. 

Kamanda Malimi amesema watuhumiwa hao wa ujambazi, wawili walikamatwa na kuhojiwa kisha kukiri kufanya uhalifu huo ambao ni Shaaban Mangote (40) mkazi wa kijiji cha Midaho na Erick Samson (19) raia wa Muyinga nchini Burundi anayeishi Benako wilayani Ngara.

Amesema watu hao walikamatwa Machi 11, 2019  eneo la Kiraka Cheusi kijiji cha Nyamalagala na baada ya kuhojiwa walikubali kwenda na polisi kuwaonyesha silaha inayotumika katika uhalifu lakini walishambuliwa na kijana aliyekuwa na silaha katika bonde la pori eneo la Ngazi kata Nyakahura .

Amesema katika mashambulizi hayo baina ya polisi na jambazi mmoja aliyekuwa porini, wawili waliokamatwa walitaka kutoroka ndipo polisi walipowajeruhi akiwemo huyo mwingine ambaye hakutambulika jina lake anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 20-23.

Aidha amesema baada ya kupatikana bunduki ya kivita AK 47 pia katika bonde la pori hilo la Ngazi Saba, pia ilikutwa magazine yenye risasi nane na maganda ya risasi matano na watuhumiwa hao walipoteza maisha wakati wakipelekwa Hospitali ya Biharamulo lakini mmojawapo hakuweza kutambulika.

"Tunawaomba wananchi wazalendo watupatie taarifa za watu wanaojihusisha na uhalifu ukiwemo ushirikiano na sisi kama jeshi la kulinda raia na mali zao tutahakikisha wanafuatiliwa na kukamatwa kisha kufikishwa mahakamani," amesema Kamanda Malimi.

Mkuu wa wilaya ya Biharamulo, Saada Malunde ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo amewahimiza viongozi wa vijiji, kuwatambua wageni wanaoingia maeneo yao na kutambua kazi zao ili kudhibiti matukio ya uhalifu.



Chanzo: mwananchi.co.tz