Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi K’njaro wamshikilia mwenzao kifo cha bodaboda

55719 POOLIUS+PC

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Wakati familia ya marehemu Waziri Zahri (20), anayedaiwa kufa akiwa mikononi mwa polisi ikidai wanazo taarifa alipigwa hadi kupoteza maisha, polisi mkoani Kilimanjaro imesema inaendelea kumshikilia askari wake mmoja kwa uchunguzi.

Ndugu wanadai kijana huyo alikamatwa na polisi Aprili 21 akiwa na afya njema na kupelekwa kituo cha Polisi Kisangara wilayani Mwanga ambako inadaiwa alipigwa hadi kupoteza maisha.

Mwili wa kijana huyo aliyekuwa dereva bodaboda ulichukuliwa na familia kwa ajili ya mazishi Mei Mosi, baada ya kuridhishwa na majibu ya kitabibu wanayodai kuwa yalionyesha kuwa alipigwa.

Kaimu kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Koka Moita aliliambia Mwananchi kuwa bado wanaendelea kumshikilia askari anayetuhumiwa kuhusika na tukio hilo huku uchunguzi ukiendelea.

“Majibu ya uchunguzi wa marehemu ni kweli yametoka, ila binafsi sijayaona lakini Jeshi la Polisi bado tunaendelea kumshikilia askari wetu na uchunguzi unaendelea,” alisema Moita.

Akizungumza na gazeti hili, mlezi wa kijana huyo, Miaya Abdi alisema walikubali kuchukua mwili kwa ajili ya maziko baada ya kuridhishwa na taarifa ya kifo.

“Hivyo sisi familia tumeridhika na majibu hayo kwamba amekufa kwa sababu ya kipigo ambacho kilisababisha majeraha mbalimbali,” alisema Abdi.

Awali, mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Thomas Apson alinukuliwa na gazeti hili akidai kijana huyo alianguka kwa kifafa wakati akiingizwa mahabusu na alikimbizwa hospitali ambako alipoteza maisha.



Chanzo: mwananchi.co.tz