Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi Arusha wakamata majambazi wakijiandaa kufanya uhalifu

ARUSHA.jpeg Polisi Arusha wakamata majambazi wakijiandaa kufanya uhalifu

Thu, 7 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

JESHI la Polisi mkoani Arusha limefanikiwa kuzima jaribio la uhalifu baada ya kuwakamata watuhumiwa wa ujambazi wanne akiwemo mganga wa kienyeji wakiwa na bunduki moja aina ya Shortgun iliokatwa kitako cha mtutu pamoja na bastola aina ya Chinese iliyofutwa namba.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Mei 7, 2020 Jijini Arusha,Kamanda wa Polisi mkoa huo Jonathan Shana, amesema watuhumiwa hao walikamatwa Mei 6 mwaka huu, majira ya saa 4:00 usiku huko eneo la daraja la Mto Nduruma Kata ya Baraa katika Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Steve Godfrey (32) mfanyabiashara na mkazi wa Tabata Jijini Dar es Salaam,Yunusi Hamed (37) mfanyabiashara na mkazi wa Korogwe mkoani Tanga.

Wengine ni Said Hamisi (38) mfanyabiashra na Mkazi wa Dar es salaam na Mganga wa kienyeji Msafiri Yohana (22) mkazi wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza.

Kamanda Shana amesema jeshi hilo lilipata taarifa za siri na waliweka mtego wao ambao ulifanikiwa kuwatia nguvuni.

Amesema watuhumiwa hao walikuwa wanatokea Dar es salaam kwenda mkoani Arusha kwa kutumia gari aina ya Toyota Crown lenye namba za usajili T.777 DSJ.

"Nia ya majambazi haya ilikuwa wanataka kufanya uhalifu hapa jijini Arusha,lakini kikosi kazi kabambe tuliweka mtego eneo la Mto Nduruma na ulipofika muda tulioambiwa tuliona gari hili linapita na askari wangu walipojaribu kulisimamisha gari hilo waliongeza mwendo mkali na askari wakaamua kufyatua risasi kupiga tairi za gari hilo na likakosa mwelekeo likagonga kingo za mto huo,"amesema

Amesema baada ya kugonga kingo hizo lilisimama, huku Yohana ambaye ni mganga wa kienyeji akiwa ametoa mikono yake nje ya madirisha akiwaonyesha chupa yenye dawa hali iliyolazimisha askari kumjeruhi kwa risasi mikono hiyo, huku wenzake wakishuka huku wamenyosha mikono juu kama ishara ya kujisalimisha.

"Tulipowapekua ndani ya gari tukakuta Shotgun moja, Bastola moja, Risasi nne za bunduki ya Shortgun,risasi nane za bastola zilizokuwa kwenye magazine,mikasi mitatu ya kukatia vyuma,nondo mbili na gundi na madawa mbalimbali ya mitishamba,"amesema.

Amesema baada ya kukamata vitu hivyo na kuwahoji watuhumiwa hao walikiri kuja Arusha kufanya uhalifu kwa kusaidiana na mganga huyo ili wasionekane.

Pia walimtaja mwenyeji wao ambaye aliwaita waje wafanye uhalifu kwa pamoja mkoani hapa.

"Wakasema hata alipokua anaonyeshea kile kichupa askari wetu waliamini askari watasinzia na hawatawaona maana ndio wanavyotumia huko walikofanya uhalifu, Morogoro,Tanga,Dar es Salaam na Mwanza,"amesema.

Ametoa wito kwa watu wote wenye nia ya kufanya uhalifu mkoani Arusha kuacha kwa sababu hawatafanikiwa na hata mwenyeji wao watamkamata wakati wowote.

"Mtaingia salama lakini hamtatoka salama sababu jeshi langu limejipanga vizuri na watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani wakati wowote,"alisema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo aliwapongeza askari hao na kuomba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Simbachawene na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) kuwaangalia askari na Kamanda wao Shana, waliofanikisha kukamatwa kwa majambazi hayo na silaha.

"Mkoa huu wa kitalii ukiingia kufanya uhalifu hauwezi toka salama sababu tumejipanga kulinda sifa ya mkoa wetu,"alisema Gambo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live