Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi Arusha wadaiwa kutesa wadhamini

034891ea2638e779c264ba7efdbd173d.jpeg Polisi Arusha wadaiwa kutesa wadhamini

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

POLISI wa Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Arusha wanatuhumiwa kuwapiga na kuwatesa wananchi wanaojitokeza kudhamini washitakiwa wanne katika kesi ya uhujumu uchumi.

Washitakiwa hao wanadaiwa kuwepo katika mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo kwa zaidi ya miezi 10 wakati dhamana yao iko wazi.

Wakati washitakiwa wakiwasilisha malalamiko hayo mahakamani, Hakimu Mfawidhi Mkoa wa Arusha, Martha Mahumbuga, alisema dhamana iko wazi na yeye ametimiza wajibu kwa mujibu wa sheria.

Mahumbuga alisema hana taarifa kuhusu kukamatwa kwa wadhamini au kwa nini wanakamatwa.

Alisema, dhamana iko wazi kwa washitakiwa wote na kama kuna wadhamini taratibu zizingatiwe ili kila mmoja atimize wajibu wa kisheria.

Washitakiwa hao ni Stephen Mhando (32) mkazi wa Tabata Dar es Salaam, Yunus Hamed (37) wa Korogwe,Tanga Said Hamisi (38,) mkazi wa Kariakoo, Dar es Salaam na Msafiri Yohana (22) aliyedaiwa kuwa mganga wa kienyeji mkazi wa Magu mkoani Mwanza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alipoulizwa kuhusu Polisi kukamata wadhamni, kuwaweka rumande na kuwatesa alisema hana taarifa kuhusu hilo na aliahidi kulifuatilia jalada la kesi hiyo na kutoa taarifa.

Inadaiwa kuwa, mbali ya kupigwa na kuteswa pia wadhamini hao hunyang'anywa mali zikiwemo simu, fedha, vitu vya thamani na kuwekwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha.

Washitakiwa katika kesi hiyo walikamatwa kati ya Mei 3 na 4 mwaka jana kwa nyakati tofauti.

Mei 7, mwaka jana, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana alitangaza kuwa walikamatwa katika Daraja la Nduruma wakati wakijiandaa kwenda kufanya ujambazi mkoani humuo.

Katika tangazo hilo alililotoa mbele ya waandishi wa habari, Kamanda Shana ambaye kwa sasa ni marehemu, alisema watuhumiwa hao walikuwa katika gari aina ya Toyota Crown lenye namba za usajili T777 DSJ wakiwa na nia ovu ya kufanya ujambazi.

Mei 8 mwaka jana watuhumiwa hao walipofikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa mbele ya Hakimu Mfawidhi Martha Mahumbuga, walisomewa shitaka la uhujumu uchumi katika Kesi Mamba 39/2020.

Dhamana ilikuwa wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili, mmoja akiwa mtumishi wa serikali.

Inadaiwa kuwa, wadhamini waliokuwa wakijitokeza ndani ya muda huo wa miezi 10 kila walipofika mahakamani, polisi waliwakamata, waliwapiga, kuwatesa na hata kutishia kuwaua.

Mmoja wa wadhamini hao ambaye ni mtumishi wa serikali na jina lake linahifadhiwa kwa sasa, alidai kuwa alikamatwa alipofika mahakamani kumdhamini mmoja wa watuhumiwa na aliwekwa mahabusu kwa siku saba katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Arusha.

Chanzo: www.habarileo.co.tz