Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Polisi 2 kortini tuhuma utoroshaji wa dhababu

D0651e53beb07b6c5cac57de5be7d759 Polisi 2 kortini tuhuma utoroshaji wa dhababu

Sat, 12 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imewafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya watuhumiwa watatu, kati ya watano, wanaokabiliwa na kesi ya utoroshaji dhababu, wakiwemo askari wawili wa Jeshi la Polisi.

Watu hao walishiriki kwenye tukio hilo lililotokea wilayani Chunya mkoani hapa hivi karibuni.

Waliofikishwa mahakamani jana ni askari wa Jeshi la Polisi, E.8970 Koplo Hassan Njujilo ambaye ni mshitakiwa namba moja na na mwenzie, G.7757 Konstebo Daniel Mrema ambaye ni mshitakiwa namba mbili.

Mwingine ni mchimbaji mdogo wa madini wilayani Chunya, Hamdun Mtafuni.

Wengine wawili wanaoendelea kutafutwa ili wafikishwe mahakamani hapo ni wafanyabiashara wakubwa wa madini, mshitakiwa namba nne, Sabra Ally na mshitakiwa namba tano, Malof Nassor.

Walifikishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, John Msafiri.

Wakili wa Serikali Mkuu na Mkurugenzi wa utaifishaji mali zinazohusu uhalifu na uhalifu unaovuka mipaka, Paul Kadushi alidai mbele ya hakimu Msafiri kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo Novemba 25 mwaka huu wilayani Chunya. Kadushi alikuwa akisaidiwa na Mkuu wa Mashitaka wa Serikali wa Mkoa wa Mbeya, Saraj Iboru.

Kadushi alidai kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo Novemba 25 mwaka huu wilayani Chunya.

Alitaja makosa saba yanayoambatana na kesi hiyo ni kujihusisha na mtandao wa uhalifu kinyume na Kifungu 4(i) (d) nne cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa.

Shtaka hilo linahusu washitakiwa namba moja na namba mbili ambao ni askari. Wanadaiwa kufanya hivyo kwa lengo la kuendeleza malengo ya genge la uhalifu wa kufanikisha utoroshaji wa madini.

Kosa la pili ni kujihusisha na genge la uhalifu kwa washitakiwa wanaobakia, mshitakiwa wa tatu, wa nne na wa tano, ambao ni wafanyabiashara wa madini.

Kosa la tatu la kupokea rushwa linawahusu askari hao wawili na mshitakiwa namba tatu, mfanyabiashara Hamduni . Wanadaiwa kuomba rushwa ya Sh milioni 150 na waliipokea. Kosa la tatu ni kupokea rushwa na kosa la nne ni la kutoa rushwa la hilo linawahusu washitakiwa namba nne na namba tano.

Kosa la sita ni matumizi mabaya ya nafasi, linalowahusu askari polisi wawili ambao ni watumishi wa umma. Wanadaiwa kukiuka Kifungu cha 31 cha sheria hiyo. Pia wanadaiwa kufanya kosa la uhujumu uchumi.

Kosa lingine ni utoroshaji wa madini nje ya nchi kinyume na sheria na hilo linawahusu wafanyabiashara. Kosa lingine ni utakasishaji wa fedha haramu na hilo linawahusu washitakiwsa wote.

Kadushi ilitoa maombi mawili kwa mahakama, ambayo ni kutoa hati ya kukamatwa kwa washitakiwa namba nne na namba tano wa kesi hiyo. Ombi la pili ni mahakama kupanga tarehe ya kesi hiyo kutajwa.

Hakimu Msafiri alitoa hati ya kukamatwa kwa washitakiwa wawili waliokimbia wakati upelelezi ukiendelea. Alisema kesi hiyo itatajwa Desemba 23 mwaka huu.

Washitakiwa wote watatu walirudishwa rumande na hawakutakiwa kujibu chochote mahakamani.

Chanzo: habarileo.co.tz