Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Plea bargaining kaa la moto

Pesa Fedhaddd Plea bargaining kaa la moto

Sun, 5 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dar es Salaam. Licha ya mapendekezo kadhaa kuelekeza uchunguzi dhidi ya utaratibu wa kukiri makosa kwa hiari (Plea Bargaining), waathirika wa utaratibu huo wameonyesha hofu wa suala hilo kutekelezwa.

Baadhi ya waathiriwa hao wanaeleza kuwa kumekosekana utashi wa kisiasa wa kuchukua hatua za kiuchunguzi dhidi ya utaratibu huo uliokuwa unasimamiwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Mapendekezo ya uchunguzi huo yalitolewa Alhamisi wiki hii bungeni na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), iliyotaka ufanyike kwa kuzingatia masharti ya sheria na Katiba ili wahusika wachukuliwe hatua.

PAC kupitia Makamu Mwenyekiti wake, Japhet Hasunga ilisema: “Serikali ifanye uchunguzi wa kina na mahususi katika suala hili kwa kuzingatia masharti ya Katiba na sheria ili wahusika wachukuliwe hatua ipasavyo kwa dosari zilizojitokeza katika mchakato huu.”

Pendekezo la PAC halikuwa la kwanza, Ripoti ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, iliwahi kufanya hivyo, ikiitaka mamlaka ya uteuzi wa aliyekuwa DPP (bila kumtaja jina) iunde tume ya kuchunguza matumizi mabaya ya ofisi yake.

Aliyekuwa DPP wakati huo ni Biswalo Mganga, ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu.

“Napendekeza mamlaka za uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ziunde tume huru ya kuchunguza uwezekano wa ukiukwaji wa maadili na matumizi mabaya ya ofisi ya umma katika mchakato wa makubaliano ya kukiri kosa,” alieleza CAG katika ripoti yake.

Katika uchunguzi wake, Kichere alibaini Sh6.1 bilioni zilizokusanywa kupitia utaratibu huo, ziliwekwa kimakosa kwenye akaunti tofauti na ile ya Plea Bargaining.

Mbali na hizo, alisema ukaguzi huo pia, ulibaini jumla ya Sh1.3 bilioni zilizokusanywa ziliwekwa hazina bila kupitia katika akaunti ya Plea Bargaining. Si hivyo tu, alieleza hakukuwa na ushahidi kwenye kitabu cha fedha wala risiti za mapokezi ya fedha hizo.

Malalamiko dhidi ya utaratibu huo, yalitolewa hata na Rais Samia Suluhu Hassan, alipozindua tume ya kurekebisha mfumo wa haki jinai jijini Dodoma. Alisema:

“Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kulikuwa na ngoma kubwa inachezwa, mpaka kukusanya fedha za wale wa Plea Bargaining. Fedha zile nyingine zinaonekana na nyingine hazionekani. Uki-trace (ukifuatilia) utaambiwa kuna akaunti China, sijui zimepelekwa pesa zipi. Tukatizame haya yote kuna nini hasa kilichoikumba Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.”

Kauli za waathiriwa

Akizungumza na Mwananchi juzi, mwanahabari, Erick Kabendera, aliyewahi kuathiriwa na utaratibu huo, alisema pamoja na mapendekezo ya PAC na mamlaka nyingine zilizowahi kuzungumzia hilo, kuna ishara ya kukosekana utashi wa kisiasa juu ya uamuzi huo.

“Kuna woga kwamba watu wanaoweza kukamatwa kwa makosa waliyoyafanya, inaweza kuleta shida kisiasa,” alisema.

Lakini alisema kutofanyika kwa uchunguzi na hatua dhidi ya utaratibu huo, kunaendelea kuacha makovu kwa wananchi, hasa wale waliowahi kuumizwa nao.

“Kuna mambo matatu hapa, CAG alipendekeza, Rais aliwahi kusema hizi fedha zimefichwa China, ile tume ya kurekebisha mfumo wa haki jinai ilipendekeza uchunguzi pia, kinachokosekana ni utashi wa kisiasa,” alisema.

Alisema uzoefu unaonyesha nchi zilizopitia madhila kama ya Tanzania, yasiporekebishwa kuna uwezekano wa kujirudia siku zijazo. Aidha, Kabendera alionyesha kushangazwa na hatua ya baadhi ya watu walioonekana kuhusika na utaratibu huo, kurudishwa kwenye mifumo ya Serikali na chama kushika nafasi mbalimbali.

Kwa upande wake, Tito Magoti, ambaye naye alipitia masaibu ya utaratibu huo, alieleza kukubaliana na mapendekezo ya PAC, akisisitiza suala hilo haliwahusu walioathiriwa na Plea Bargaining pekee, bali wananchi wote.

Kwa mujibu wa Magoti, ambaye ni mwanaharakati wa haki za binadamu, iwapo suala hilo litatekelezwa, litajenga taswira njema ya Mahakama kwa umma na lisipotekelezwa itakuwa kinyume chake.

Uchunguzi dhidi ya jaji

Alipoulizwa kuhusu utaratibu wa uchunguzi dhidi ya jaji, Jaji Kiongozi mstaafu, Amir Manento alisema zipo taratibu zinazopaswa kufuatwa.

Alisema uchunguzi dhidi ya jaji unapaswa kufanywa na tume ya maadili ya kiongozi huyo inayoundwa na majaji wenzake.

Manento alisema kamati hiyo huundwa na majaji watatu na wawili kati yao wanapaswa kutoka katika nchi za Jumuiya ya Madola.

“Mwenyekiti wa kamati anapaswa kutoka katika moja ya nchi hizo na wajumbe hawapaswi kuwa miongoni mwa watu watakaokuwa na masilahi au hofu dhidi ya anayechunguzwa,” alisema.

Alisema hilo hufanyika ili kulinda uhuru wa Mahakama na kuepusha mgongano wa masilahi katika uchunguzi husika.

“Mjumbe wa tume hiyo hapaswi kuwa mmoja wa wale ambao pengine atakuwa na hofu ya kupoteza ajira yake kwa kumchunguza jaji husika au vinginevyo,” alisema. Alisema mkuu wa nchi hawezi kuunda tume hiyo, kwa kuwa hata ajira ya jaji, haitokani naye moja kwa moja.

Kwa upande wake, Jaji kiongozi mstaafu, Fakih Jundu, alisema taratibu hizo zitafuatwa iwapo tuhuma za jaji husika hazihusishi jinai.

Kama zinahusisha jinai, alifafanua jaji husika atachunguzwa kwa utaratibu kama ambavyo wananchi wengine huchunguzwa, isipokuwa mamlaka za Mahakama lazima zijulishwe.

Kulingana na Jaji Jundu, iwapo tuhuma zinahitaji kumuondoa kiongozi huyo kwenye nafasi yake, lazima kuundwe kamati itakayohusisha majaji kutoka nje ya Tanzania.

“Kama anataka kuondolewa kwenye nafasi yake lazima kuwe na kamati yenye majaji kutoka ndani na nje ya nchi, hao watachunguza tuhuma husika kisha itaonekana nini cha kufanya,” alisema.

Magoti akizungumzia hilo, alisema upo utaratibu wa kuwachunguza majaji ulioainishwa katika Ibara ya 110 (6) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ibara hiyo inaeleza: “Iwapo Rais anaona kuwa suala la kumwondoa Jaji kazini linahitaji kuchunguzwa, basi katika hali hiyo mambo yatakuwa ifuatavyo:

(a) Rais atateua Tume ambayo itakuwa na mwenyekiti na wajumbe wengine wasiopungua wawili. Na huyo mwenyekiti na angalau nusu ya wajumbe wengine wa Tume hiyo itabidi wawe watu ambao ni majaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani katika nchi yoyote iliyomo kwenye Jumuiya ya Madola.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live