Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pingamizi la anayedaiwa kuvamia Kanisa la RC Geita latupwa

Kanisa Rc Geita D Pingamizi la anayedaiwa kuvamia Kanisa la RC Geita latupwa

Tue, 25 Apr 2023 Chanzo: mwanachidigital

Jitihada za awali za mshtakiwa Elpidius Edward kujinasua kutoka kwenye kesi ya kuingia kwa jinai ndani ya Kanisa Katoliki Jimbo la Geita na kusababisha uharibifu wa mali zenye thamani ya Sh48.2 milioni zimekwama baada ya Mahakama kutupilia mbali pingamizi lake.

Mshtakiwa huyo anayekabiliwa kesi namba 62/2023 mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita aliweka pingamizi akiiomba Mahakama kutopokea kama kielelezo nyaraka yenye orodha ya mali yenye thamani ya Sh48.2 milioni zinazodaiwa kuharibiwa wakati wa tukio lililotokea Februari 26, mwaka huu.

Kielelezo hicho kiliwasilishwa mahakamani na shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, Elias Masolwa ambaye pia ni Makamu wa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita.

Kabla kuomba kuitoa orodhas hiyo ya mali iliyoharibiwa kama kielelezo, shahidi huyo aliiambia Mahakama jinsi alivyopokea taarifa za uvamizi na uharibifu uliofanyika kanisani.

Akitoa uamuzi kuhusu pingamizi hilo leo Jumanne Aprili 25, 2023, Hakimu Mkazi Geita, Johari Kijuwile ametupilia mbali pingamizi hilo akisema halina mashiko kisheria na kupokea orodha hiyo ya mali kama kielelezo namba moja cha upande Jamhuri.

Mshtakiwa Elpidius, mkazi wa mtaa wa Katundu Wilaya ya Geita anashtakiwa kwa makosa mawili ikiwemo la kuingia katika jengo la Kanisa Katoliki Geita kinyume na kifungu cha 294 (1) na (2) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Katika shtaka la pili, mshatakiwa huyo anadaiwa kuharibu mali zenye thamani ya Sh48.2 milioni kinyume cha kifungu namba 226 (1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 na marejeo ya mwaka 2022.

Shauri hilo limeahirishwa hadi Mei 10, 2023 litakapoendelea kwa upande wa mashtaka kuita mashahidi wengine.

Mshtakiwa amerejeshwa mahabusu kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya fedha taslimu Sh24.1 milioni au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.

Chanzo: mwanachidigital