Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Picha ya hukumu ya kina Mbowe kortini leo

98503 Mbowe+pic Picha ya hukumu ya kina Mbowe kortini leo

Tue, 10 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watapona au watanaswa? Pengine hili ni swali linalogonga vichwa vya viongozi saba wa Chadema na kada mmoja wa CCM wakati hukumu ya kesi ya jinai inayowakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ikitarajiwa kusomwa leo.

Swali hili linaweza lisiwe kwa washtakiwa hao tu, bali hata kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, wanachama wa Chadema, wadau wa masuala ya siasa na wananchi kwa ujumla ambao wamekuwa wakifuatilia kesi hiyo.

Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba. Kwa mujibu wa kifungu cha 63B cha Sheria ya Kanuni za Adhabu (Penal Code-PC), washtakiwa wanaopatikana na hatia ya uchochezi, dhidi Jamhuri, adhabu yake ni faini isiyozidi Sh1,000 au kifungo cha miezi 12 jela au vyote kwa pamoja.

Katika kesi hiyo Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai, Kilimanjaro na wenzake ambao wengi wao pia ni wabunge, wanakabiliwa na mashtaka 13, likiwemo ya kula njama, kufanya mikusanyiko na maandamano yasiyo halali na kuchochea uasi.

Mbali na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, wengine katika kesi hiyo Katibu mkuu wa Chadema pia mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Salum Mwalimu (naibu katibu mkuu - Zanzibar) na Peter Msigwa (mbunge wa Iringa Mjini na mwenyekiti kanda ya Nyasa).

Pia wamo Esther Matiko (mbunge wa Tarime mjini na mwenyekiti Kanda ya Serengeti), Halima Mdee (mbunge wa Kawe pia mwenyekiti wa Baraza la Wanawake), Esther Bulaya (mbunge Bunda), John Heche (mbunge wa Tarime Vijijini) na katibu mkuu mstaafu, Dk Vicent Mashinji, aliyehamia CCM.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 16, 2018 katika viwanja vya Buibui na barabara za Kawawa na Mkwajuni wilayani Kinondoni wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Kinondoni.

Katika hukumu ya leo kama ilivyo kawaida kwa kesi zenye washtakiwa zaidi ya mmoja, kuna matokeo ya aina tatu yanayoweza kutokea; washtakiwa wote kutiwa hatiani, washtakiwa wote kuachiwa huru au baadhi kupatikana na hatia na wengine kutokutwa na hatia.

Hii inatokana na aina ya mashtaka yanayowakabili washtakiwa ambao wako katika makundi matatu kwa kuzingatia mashtaka yanayowakabili. Kwanza ni wale wanaoshtakiwa kwa makosa ya kufanya mkusanyiko na maandamano yasiyo halali.

Pili wale wanaoshtakiwa kwa kutoa maneno ya uchochezi kwenye mkutano wa kufunga kampeni.

Kundi la tatu ni wale wanaoshtakiwa kwa kufanya mkusanyiko na maandamano yasiyo halali.

Washtakiwa wote katika utetezi wao walikana mashtaka na wengine walitoa utetezi unaoitwa kwa lugha ya kisheria “alibi” (alibai) kwamba hawakuwapo eneo la tukio, ilhali wakikabiliwa na mashtaka ya mkusanyiko na maandamano yasiyo halali.

Lakini hata wale wanaokabiliwa na mashtaka ya uchochezi pia walikana kutoa maneno ya uchochezi huku wakidai kuwa yalikuwa ni maneno ya kawaida ambayo hayana tatizo.

Kisheria wajibu wa kuthibitisha mashtaka ili kuwatia hatiani washtakiwa ni wa upande wa mashtaka. Katika kesi za jinai kama hii, kiwango cha kuthibitisha mashtaka ni kutokuacha mashaka yoyote.

Hii ina maana kwamba hata kama utetezi wa washtakiwa utakuwa dhaifu, kutiwa hatiani kutategemea uzito wa ushahidi wa upande wa mashtaka. Kwa hiyo upande wa mashtaka unapaswa uwe umethibitisha, kwanza washtakiwa waliokana kuwepo kwenye mkusanyiko na maandamano wanayodaiwa kuyafanya isivyo halali, kupitia ushahidi wa mashahidi wake na au vielelezo vya ushahidi walivyoviwasilisha mahakamani.

Pia upande wa mashtaka unapaswa uwe umethibitisha kuwa washtakiwa walitoa maneno yanayodaiwa kuwa ya uchochezi. Hati ya mashtaka imebainisha maneno aliyoyatoa kila mshtakiwa yanayodaiwa kuwa ni ya uchochezi.

Lakini kubainisha maneno hayo ni jambo moja na ni rahisi lakini kazi kubwa kwa upande wa mashtaka ni kuthibitisha kuwa maneno hayo ni ya uchochezi.

Hapa vifungu vya sheria wanavyoshtakiwa navyo vitahusika sana ili kupata tafsiri ya uchochezi na kuona kama maneno hayo wanayodaiwa kuyatoa yanakidhi vigezo vya kisheria kuwa maneno ya uchochezi.

Mbali na tafsiri hiyo ya vifungu vya kisheria, pia mahakama katika hukumu yake itakuwa imerejea hukumu za kesi mbalimbali zilizokwisha kuamriwa na au mahakama hiyo yenyewe au mahakama za juu yake zenye mazingira yanayofanana na kesi hii.

Hivyo katika hukumu hiyo itachambua ushahidi dhidi ya kila mshtakiwa kuonyesha namna ulivyomgusa au kutokumgusa na kulinganisha na utetezi wake na hapa ndipo matokeo hayo matatu yanaweza kujitokeza katika hukumu hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz