Dar es Salaam. Washtakiwa wawili akiwemo mfanyabiashara Marijan Msofe maarufu Papa Msofe wameunganishwa katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili wakili wa kujitegemea, Abdul Lyama.
Msofe na Fadhili Mganga wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu dola 26, 250 za Kimarekani sawa na zaidi ya Sh60 milioni.
Wakili wa Serikali, Grory Mwenda akisoma hati ya mashtaka leo Jumanne Februari 11, 2020 mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Kisutu, Augustina Mmbando amedai washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka la kuunda genge la uhalifu, utakatishaji fedha na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Mwenda amedai kati ya Januari Mosi, 2019 na Desemba 30, 2019 jijini Dar es Salaam washtakiwa waliunda genge la kihalifu huku akijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.
Katika shtaka la pili, wanadaiwa tarehe hiyohiyo jijini Dar es Salaam walijipatia dola 26, 250 za kimarekani sawa na zaidi ya Sh60 milioni wakijua fedha hizo ni zao la jinai la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Shtaka la mwisho wanadaiwa tarehe hiyo jijini Dar es Salaam washtakiwa walijipatia dola 26, 250 za kimarekani sawa na zaidi ya Sh60 milioni kutoka kwa Yasser Moawed Abdelhamad wakimdanganya kumuuzia tani 25 za madini ya Shaba huku wakijua siyo kweli.
Habari zinazohusiana na hii
- Papa Msofe afutiwa kesi ya mauaji
- Mfanyabiashara mwingine Tanzania aunganishwa kesi ya 'Papa Msofe'
- Kilichotokea mahakamani kesi ya 'Papa Msofe'
- Papa Msofe na wenzake kortini wakidaiwa utakatishaji fedha
Hakimu Mmbando ameahirisha shauri hilo hadi Februari 25, 2020 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Msofe anakabiliwa na kesi nyingine pamoja na wenzake watano. Wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kujipatia Sh943 milioni kwa njia ya udanganyifu.