Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Padri: Ushabiki wa vyama vya siasa unavuruga ndugu, jamii

34122 Siasa+pic Tanzania Web Photo

Mon, 31 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serengeti. Watanzania wametakiwa kuachana na siasa za chuki kwa kuwa zimechangia jamii na Taifa kupoteza upendo.

Akihubiri katika Misa ya familia Takatifu katika Kanisa Katoliki la Mugumu leo Jumapili Desemba 30, 2018 Padri Paslei Ghati amesema siasa zimefikia hatua ya kuvuruga ndoa na kuchangia malezi mabaya ya watoto.

"Mtu wa chama fulani hawezi kuoa wa chama fulani, hii ni hatari kubwa, inabidi yaangaliwe vizuri maana tunagawa taifa na dhambi hiyo inaathiri ndoa nyingi na waathirika ni watoto," amesema.

Amesema familia bora zinazozingatia mafunzo ya Mungu zinazaa viongozi bora, hivyo tofauti za kisiasa zisitumike kugawa watu bali kuwaunganisha kwa pamoja.

"Imefika wakati uchumba unavunjika, ndoa zinaingia migogoro sababu huyu ni chama fulani na huyu chama fulani, tusiruhusu chuki hiyo itamalaki maana athari yake ni kubwa leo na hata baadaye," amesema.

Kiongozi  huyo wa kiroho amewataka waumini na Watanzania kwa ujumla kuiga mfano wa familia ya Yesu, Maria na Yosefu ilivyokuwa na umoja.

"Kwa mjibu wa maandiko Yesu alijua yeye ni mkuu kuliko Maria na Yosefu lakini alijishusha na kuwasikiliza, hayo ndiyo tunatakiwa kuyaishi kwa kutanguliza utii kwa Mungu badala ya mambo yanayotugawa kifamilia na Kitaifa," amesema.

Kuhusu athari za mvurugano ndani ya familia amesema hali hiyo husababisha watoto hukosa malezi na matokeo yake wanajiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya, ndoa za jinsia moja na ushoga.

Amewataka vijana kuacha kuiga utamaduni wa mataifa ya nje ambao unatweza utu wa Watanzania, alitaja mambo mabaya yanayoigwa na vijana kuwa ni mavazi yasiyo na staa, ulevi na hata kutoheshimu wazazi.



Chanzo: mwananchi.co.tz