Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Padri Soka apangua kesi nyingine ya ubakaji

Padri Soka Ubakaji.png Padri Soka apangua kesi nyingine ya ubakaji

Wed, 27 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Padri Sosthenes Soka (42) wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi ameendelea kupangua kesi za ubakaji zinazomkabili baada ya jana kuachiwa huru katika kesi ya pili.

Septemba 22, 2023 mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi ilimwachia padri huyo katika kesi namba 44 ya mwaka 2022 baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha shtaka la kubaka mtoto wa miaka 12 kwa viwango vinavyokubalika kisheria.

Zikiwa zimepita siku nne, Hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama hiyo, Herieth Mhenga jana alimwachia huru Padri Soka katika kesi namba 45 ya 2022 ya tuhuma za kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 12 bila ruhusa yake.

Kama ilivyokuwa kesi namba 44 ya 2022, Hakimu huyo alisema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shtaka dhidi ya mtuhumiwa huyo kuwa Agosti 12, 2022 akiwa katika kanisa hilo, alimbaka mtoto huyo wa miaka 12.

Hakimu Mhenga alieleza kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kudhibitisha shtaka na kwamba kumekuwa na mashaka mengi katika ushahidi wa upande wa mashtaka, ambayo umeshindwa kuyatolea majibu.

Pia alisema kulikuwa na kutofautiana kwa maelezo ya mashahidi, hivyo kupelekea ushahidi wao kutotiliwa maanani na mahakama hiyo.

"Mshtakiwa aliieleza mahakama wakati tukio linatendeka hakuwepo eneo hilo na upande wa mashtaka umeshindwa kupinga utetezi wa padri na kupelekea mahakama kuamini kuwa mshtakiwa hakuwepo eneo la tukio kama inavyodaiwa na upande wa mashtaka," alisema Hakimu.

Hata hivyo, Hakimu Mhenga ameeleza kuwa kulikuwepo na mashahidi muhimu ambao upande wa mashtaka ulitakiwa kuwaleta mahakamani lakini ulishindwa kufanya hivyo na haukueleza chochote mahakamani hapo ni kwanini mashahidi hao hawakwenda kutoa ushahidi wao.

Hivyo kutokana na ushahidi uliotolewa, mahakama imefikia uamuzi kuwa mshtakiwa hana hatia na hivyo kumwachia huru katika kesi hiyo iliyokuwa na mashahidi 7 na vielelezo vitano, ikiwemo PF3 ya mwathirika wa tukio hilo.

Padri Soka aliyekuwa anahudumu katika Kanisa la Mt Dionisi Aropagita lililopo Kawawa Mjini Moshi, alikamatwa Septemba 20, 2022 na kufikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Septemba 26 na kufunguliwa kesi tatu tofauti za kubaka watoto watatu na kwa hukumu hiyo, sasa amebakiwa na kesi moja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live