Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Operesheni mpya dhidi ya ‘panya road’

Kamanda Muliro Operesheni mpya dhidi ya ‘panya road’

Wed, 21 Sep 2022 Chanzo: Mwananchi

Wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla akitangaza mikakati ya kudhibiti makundi ya uhalifu ya vijana wanaojulikana kama ‘panya road’, gumzo limetawala kuhusu mtu anayedaiwa kiongozi wa moja ya makundi hayo, George Bonge maarufu kwa jina la rais wa Mabibo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Jumanne Muliro, Bonge na wenzake walikuwa wamepanga kwenda kufanya uhalifu maeneo ya Goba.

Wakiwa njiani polisi waliokuwa na taarifa juu yao wakawazingira na kuua sita kwa risasi Jumamosi usiku, katika eneo la Makongo Juu jijini hapa.

Mbali na tukio hilo, Makalla alisema watu 135 wamekamatwa ndani ya siku nne wakati wa operesheni ya kudhibiti vikundi vya uhalifu maarufu kama panyarodi.

Watu hao wamekamatwa katika operesheni iliyoanza Septemba 15 ikilenga kutokomeza vikundi vya uhalifu vilivyoibuka mwanzoni mwa Sepetemba, vikivamia mitaa mbalimbali ya jiji, kupora mali, kujeruhi na hata kuua.

Makalla alisema ulinzi unaendelea kuimarishwa katika mkoa huo na tangu kuanza kwa operesheni hiyo hakuna mipango ya tukio la uhalifu iliyofanikiwa.

“Nilitangaza Septemba 15 kuwa tumeongeza askari 300 lakini watu hawa hawakutaka kusikia, wakaenda kujaribu kule Makongo na Ubungo kilichowatokea ndio kama hivyo mlivyosikia. Walitaka kushindana na polisi wameuawa sita,” alisema Makalla.

Alisema katika siku hizi nne tumekamata vitu mbalimbali vya wizi zikiwemo runinga 23 na watuhumiwa 135 na wanaendelea kuwahoji.

Mkuu huyo wa mkoa alieleza kuwa baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa walitoa ushirikiano na kuwataja wanaonunua mali hizo, hatua iliyoliwezesha Jeshi la Polisi kuwakamata wafanyabiashara watano wanaonunua mali za wizi.

“Vijana wametoa ushirikiano ambao umewezesha kukamatwa kwa wafanyabiashara watano ambao kazi yao ni kununua mali za wizi. Sasa tunakuja na operesheni kabambe kwa wanaoendesha maduka yao kwa kutegemea mali za wizi.

“Hawa watuhumiwa wameeleza kabisa huwa wanapewa maelekezo ya bidhaa zinazohitajika. Tunaenda kushughulika na watu hawa, haiwezekani unaendesha duka kwa kutegemea bidhaa za wizi”.

Mkuu wa mkoa alitaja mkakati mwingine wa kupambana na uhalifu kuwa ni vituo vya polisi vidogo kufanya kazi kwa saa 24 na doria kuongezeka katika mitaa.

Alisema ili kufanikisha hilo, kila kata itakuwa na gari la polisi ambalo linafanya doria kwa saa 24.

“Vile vituo vilivyokuwa vinafungwa saa 12 sasa vitafanya kazi saa 24, hii ina maana kwamba polisi hawatalala na wako tayari kushirikiana na wananchi... Ulinzi utazidi kuimarishwa na tumekubaliana kila mtaa kuwa na mkutano wa wiki ya kwanza ya mwezi kujadili suala la ulinzi na usalama,” alisema Makalla.

Mkakati mwingine alioutaja ni kuongeza ufuatiliaji wa watu wanaotoka magerezani kwa kuwa imebainika kwamba asilimia kubwa ya viongozi wa magenge ya uhalifu ni watu waliomaliza vifungo vyao magerezani au kuachiwa huru kwa sababu mbalimbali.

Sababu kuua

Akizungumzia sababu za polisi kutumia silaha kupambana na wahalifu wenye mapanga, Makalla alisema, “Tutatumia maarifa yote kumaliza uhalifu. Niwaambie ‘panyarodi’ na wahalifu wote kwamba kwa mikakati tuliyoweka tutapambana nao na sisi hatupo kwa ajili ya kushindwa.

“Ukiambiwa jisalimishe tii amri, usikaidi, polisi amepewa silaha unapotaka kumjeruhi kwa panga haiwezekani, hiyo ni vita kali. Huwezi kutoka na mapanga ukapambana na polisi walio na silaha, ndiyo hayo yaliyotokea Makongo,” alisema.

Tutahakikisha usalama

Kwa upande wake Kamanda Muliro alisema kazi ya Jeshi la Polisi ni kuhakikisha wananchi wanakuwa salama, hivyo wahalifu wanapaswa kukaa chonjo.

“Tumeshaanza operesheni inayolenga kuhahakikisha wananchi wa Dar wanakuwa salama. Wahalifu wakae chonjo, tutafanya kazi kubwa ya ziada kuhakikisha wananchi wanakuwa salama lakini kazi yetu itazingatia misingi ya kisheria.”

Simulzi ya Bonge

Kufuatia taarifa za kuuawa kwa George Bonge au rais wa Mabibo, majirani zake wameeleza walivyokuwa wakiishi naye.

Akizungumza na Mwananchi mmoja wa waendesha bodaboda eneo la Mabibo, alisema wamepata taarifa za kuuawa kwa George juzi, aliyekuwa akiishi Mabibo Sahara ingawa hawakuwa na taarifa za kina za msiba wake.

“Siku zote huwa tunashinda naye hapa na alipoondoka juzi hakusema anapoenda, jana hajaonekana. Tumewasiliana na mdogo wake kasema ni kweli ameuawa lakini hatujajua msiba ulipo,” alisema dereva bodaboda.

Mkazi wa Mabibo Sahara, Sarah Tito alisema taarifa wanazozisikia ndiyo hizo kuwa George Bonge kauawa lakini hawana uhakika, kwa kuwa mtu aliyekuwa wanaishi naye amesafiri.

“Alikuwa hakauki hapa dukani kwangu, alikuwa akipita anapenda kula cripsi za mihogo, leo ni siku ya pili hatujamuona na hizi taarifa za kifo chake hatuna uhakika nazo, lakini kila mtu anaongea lake.

“Watu walimuona na bodaboda mwenzie na walivyoondoka wote hawajarudi, inawezekana hizi taarifa ni sahihi na kama angekuwepo kuna hiyo baa hapo ndiyo huwa anashinda,” alisema Sarah.

Kuhusu kujihusisha na uhalifu, Sarah alisema George aliwahi kuwa gerezani na kutoka, baadaya muda alikamatwa tena akawa ndani na ametoka muda si mrefu.

Mkazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Michael, alisema taarifa za kuuawa kwa ‘rais wa Mabibo’ zimewashtua kwa kuwa walikuwa hawajui kama ana matukio ya namna hiyo.

Mmoja wa watu waliyomfahamu George (ambaye hakutaka kutajwa gazetini), alisema alimfahamu kijana huyo kwa matukio mbalimbali ya uhalifu miaka ya nyuma na siku ya tukio alivwaaga ndugu na jamaa kwamba anaenda kwenye kazi.

Alisema siku ya tukio wakiwa na gari lao, aliaga kwao na walipofika eneo la Ubungo waliponunua viatu aina ya raba na kuanza safari kwenda Goba.

“Nilitumiwa picha zao wakiwa wanavuja damu ila niliambiwa usiku ule walikuwa hapa maeneo ya Ubungo wakanunua na viatu, wakavua vile ambavyo walivaa mwanzo,” alisema mama huyo.

Aliongeza kuwa rais wa Mabibo alifahamika kwa matukio ya wizi na unyang’anganyi kwa muda mrefu katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Mlimani City walipokuwa wakiiba kwenye magari.

“Tulikuwa tunamsihi sana aache hizi tabia ila ni kama siku yake ilifika tu inaumiza sana kwa sababu bado vijana,” alisema.

Katika eneo, gazeti hili lilishuhudia vikundi mbalimbali katika maongezi, mengi yakimhusu George Bonge.

Eneo hatari

Ukiacha Mabibo, Mwananchi limetembelea eneo la Kimwani Chanika linalodaiwa kuwa maficho ya panyarodi na kukuta wananchi wakiwa na hofu.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema eneo hilo ni hatari, limekithiri kwa kuwa na vijana wanaojihusisha na uvutaji bangi ambao kwao kumkaba mtu na kumpora ni jambo la kawaida.

Alisema kinachosikitisha zaidi ni kwamba eneo hilo lipo hatua chache kutoka Kituo cha Polisi Chanika.

“Tunaomba Serikali itupie jicho eneo hili, haiwezekani vijana wanavuta bangi waziwazi halafu hakuna hatua yoyote inayochukuliwa na polisi wapo jirani ipo namna,” alisema.

Mariam Hussein alisema haya kukiwa na sherehe katika maeneo hayo vijana hao wamekuwa wakiwalika wenzao wa maeneo mengine wanaoendana na tabia zao na huenda kuvamia bila woga.

“Yaani huko kama umealikwa sherehe ujipange kwelikweli kwa usalama wako, yaani kwa kifupi ni kama watu wa kule wapo kisiwa kingine tofauti na Tanzania,” alisema Mariam.

Kwa upande wake Jonas Josephat alisema kitendo cha kuelezwa mipango ya panyarodi inafanyikia Chanika ni kuwafanya waishi maisha ya wasiwasi.

“Kipindi cha miezi miwili wakati matukio haya ya panyarodi yalivyotokea tulikuwa hatuna raha, watu walikuwa wakikamatwa ovyo hata wasiohusika.

“Ninashauri kama vipi huku nako kufanywe Kanda Maalumu kama polisi waliopo wameshindwa kazi,” alisema Josephat.

Mwendesha bodaboda aliyejitambulisha kwa jina la Walii Mzee, alisema matukio ya panyaroad wanayasikia mjini lakini huko Chanika tangu yalivyotokea kipindi cha nyuma hawajayasikia.

Hata hivyo, alisema wizi mkubwa unaokithiri ni wizi wa pikipiki na kutaja maeneo maarufu kwa matukio hayo ni Brazilian na Day Live.

“Kila siku bodaboda tumekuwa ukiporwa pikipiki zetu maeneo haya,wizi ambao ni mkubw kuliko huo wa panya road,” alisema.

Hawatoki Kawe

Huko Kawe ambako siku za karibuni panyarodi walivamia na kuua, kumeelezwa kuwa wahalifu wengi ni wageni.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mzimuni, Kawe, Raiya Amour alisema watu wanaofanya matukio eneo hilo wengi hawatoki mitaa hiyo na matukio yanaweza kuzuilika kama kutakuwa na ushirikishwaji wa wananchi, wenye nyumba na Serikali.

Imeandikwa na Elizabeth Edward, Fortune Francis, Tuzo Mapunda na Nasra Abdallah.

Chanzo: Mwananchi