Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ofisa uhamiaji, wenzake wahukumiwa mwaka mmoja jela au kulipa Sh600,000

50277 Pic+uhamiaji

Thu, 4 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu kulipa faini ya Sh600,000 au kifungo cha mwaka mmoja jela ofisa uhamiaji wa wilaya ya Kinondoni, Emil Mponi (40) na wenzake wanne baada ya kukiri makosa yaliyokuwa yakiwakabili.

Mbali na Mponi washtakiwa wengine waliohukumiwa ni Ibrahim Sanka (29), Emmanuel Sanka (29), Geogre Mollel (24) na Peter Byakatunda (38).

Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amewatia hatiani washtakiwa hao leo Jumatano Aprili 3, 2019 baada ya kukiri makosa yaliyokuwa yakiwakabili.

Makosa hayo ni kujipatia hati ya dharura ya kusafiria, utoaji wa hati za kusafiria kinyume na utaratibu na kuwasilisha nyaraka za uongo.

Upande wa washtakiwa Ibrahim, Emmanuel na Mollel waliokuwa wakikabiliwa na shtaka la kwanza la kujipatia hati ya dharura ya kusafiria walitiwa hatiani na kuhukumiwa kulipa faini ya Sh600,000 au kutumikia kifungo cha miaka miwili jela kila mmoja.

Katika shtaka la utoaji hati za kusafiria kinyume cha taratibu ambalo mshtakiwa Mponi na Byakatunda wanadaiwa kuzitoa kwa washtakiwa Ibrahim, Emanuel na Mollel walihukumiwa kulipa faini ya Sh600,000 au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Hakimu Shahidi amewataka washtakiwa hao wajieleze kwa nini wasipewe adhabu kali. Washtakiwa hao kwa nyakati tofauti wameiomba Mahakama iwapunguzie adhabu kwa sababu hilo ni kosa lao la kwanza.

Wakili wa Serikali, Abutwalib Hamis ameiomba mahakama hiyo iwapatie adhabu kali washtakiwa hao ili iwe fundisho kwa watu wengine.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Shahidi amesema katika shtaka la pili washtakiwa Ibrahim, Emmanuel na Mollel waliwasilisha nyaraka za uongo na kujipatia hati ya dharura ya kusafiria na wote kwa pamoja walikana kutenda kosa hilo.

"Kwa kuwa washtakiwa wote watatu wamekana shtaka la pili hivyo mnatakiwa mrudi ili mpewe masharti ya dhamana siku ya kesi yenu itakapotajwa tena, kama hamjalipa faini tutaendelea na hili shauri mkitokea gerezani," alisema Hakimu Shaidi.

Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 15,2019  itakapotajwa tena.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka wakili, Hamisi amedai katika shtaka la kwanza Machi 18, 2019 washtakiwa Ibrahim, Emmanuel na Mollel walijipatia hati ya dharura ya kusafiria katika ofisi za uhamiaji wilaya ya Kinondoni kwa lengo la kutoa maelezo ya uongo wakidai wao ni wanafunzi wanamtembelea mama yao ambaye ni mgonjwa anayeishi jijini Nairobi nchini Kenya huku wakijua si kweli.

Katika shtaka la pili Machi 30,2019 katika uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere walikamatwa Ibrahim, Emmanuel na Mollel baada ya kukutwa wamewasilisha nyaraka za uongo ili kupata hati ya kusafiria katika maelezo yao waliyotoa katika ofisi ya mkoa ya uhamiaji walipohojiwa walikubali kutoa maelezo ya uongo.

Shtaka la tatu Machi 30,2019 washtakiwa Mponi na Byakatunda walikamatwa baada ya kuruhusu kutolewa kwa hati za kusafiria kwa washtakiwa Ibrahim, Emmanuel na Mollel kinyume na utaratibu kwa kuwa hawakustahili kupewa.



Chanzo: mwananchi.co.tz