Babati. Ofisa wa madini mkazi mkoa wa kimadini Simanjiro, Daudi Ntalima amefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Manyara kwa tuhuma ya kuomba rushwa ya Sh5 milioni kwa wakurugenzi wa kampuni ya Tanzanite One.
Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Eveline Onditi akisoma hati ya mashtaka leo Ijumaa Machi 6, 2020 amedai mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Februari 21, 2020.
Mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa huo, Simon Obero mwendesha mashtaka huyo amedai mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo huku akijua ni kinyume cha sheria.
Amedai kuwa mshtakiwa aliomba rushwa hiyo kwa wakurugenzi wa kampuni hiyo, Hussein Gonga na Faisal Shabahi.
Amedai alitenda kosa hilo kwenye eneo la mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Hata hivyo, hakimu Obero alipomuuliza mshtakiwa huyo kama ni kweli alitenda kosa hilo alikana mashtaka hayo.
Pia Soma
- Watalii kutoka Italia wapigwa ‘stop’ kuingia Zanzibar kuepuka maambukizi ya corona
- Majaliwa aagiza mkurugenzi bodi ya mkonge kurudishwa alikotoka
- Google, Facebook waruhusu waajiriwa wafanye kazi wakiwa nyumbani kuepuka corona
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 21, 2020 itakapotajwa tena mahakamani hapo. Mshtakiwa huyo yupo nje kwa dhamana.