Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ofisa elimu, mgambo wapandishwa kizimbani kwa rushwa

Taku Pic Ofisa elimu, mgambo wapandishwa kizimbani kwa rushwa

Mon, 5 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Ofisa elimu wa kata ya Lugubu, Daudi Joram na askari mgambo, Salumu Tinde wamefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo ya Igunga wakidaiwa kuomba na kupokea rushwa ya Sh780, 000.

Katika kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa katika Mahakama ya Mwanzo Igunga mbele ya hakimu, Jackline Kessy, washitakiwa hao wanadaiwa kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa Makala Mkoma na Godfrey Kilaziga wote wa kata ya Lugubu.

Mwendesha mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mazengo Joseph, ameiambia mahakama hiyo kuwa washitakiwa wanashitakiwa kwa makosa mawili ya kuomba rushwa na mawili ya kupokea rushwa.

Mazengo amedai kuwa Nov24, 2022 washitakiwa wote wawili wakiwa ofisi ya mtendaji wa kata ya Lugubu kwa makusudi waliomba rushwa ya Sh300, 000 kutoka kwa Makala Salumu Mkoma ili wasimchukulie hatua za kisheria kwa kosa la kumpiga mwanaye Ngolo Makala na kumsababishia majeraha mwilini.

Shitaka la pili kwa washitakiwa hao ni kwamba katika tarehe hiyo wakiwa ofisi ya kata ya Lugubu walipokea kiasi cha Sh300, 000 kutoka kwa Makala Salumu Mkoma ili wasimchukulie hatua kwa kosa hilo hilo.

Mwendesha mashitaka huyo amesema shitaka la tatu kwa washitakiwa hao wawili, katika tarehe hiyo kwa muda tofauti wakiwa katika ofisi hiyo ya kata ya Lugubu waliomba rushwa ya Sh480, 000 kutoka kwa Godfrey Kiraziga ambaye alikamatwa kwa kosa la kujihusisha kimapenzi na mwanafunzi wa shule ya msingi kata ya Itumba.

Mazengo amesema shitaka la nne kwa washitakiwa hao, katika tarehe hiyo kwa muda tofauti wakiwa katika ofisi ya mtendaji wa kata walipokea kiasi cha Sh480,000 kutoka kwa Godfrey Kilaziga ili asichukuliwe hatua kwa kosa hilo hilo.

Mazengo amesema kuwa washitakiwa wote wawili wametenda makosa hayo kinyume na kifungu 15(1a), (2) na 3(a) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.329 marejeo ya 2019 na kuongeza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Baada ya washitakiwa kusomewa mashitaka hayo manne, hawakutakiwa kujibu chochote, kwani hakimu wa mahakama ya mwanzo hana mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kutokana na hakimu wa wilaya kutokuwepo na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 14, 2022.

Mshitakiwa Daudi Mayila Joram yuko nje kwa dhamana ya Sh2 milioni wakati mwenzake Salumu Hassani, akipelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Chanzo: Mwananchi