Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ofisa elimu mbaroni madai za kumhonga ofisa Takukuru

CRIME SCENE.png Ofisa elimu mbaroni madai za kumhonga ofisa Takukuru

Sat, 25 Apr 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), inawashikilia Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mkoani hapa, Albert Ngimba, na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Isenengwa wilayani humo, George Mmembwa, kwa tuhuma za rushwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye ofisi za Takukuru mkoani hapa, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, alidai lengo la watuhumiwa hao kutenda kosa hilo ni kumshawishi ofisa huyo wa Takukuru awasaidie kwenye uchunguzi unaohusiana na tuhuma za ufujaji na ubadhirifu wa fedha zilizotolewa na serikali.

Alidai kuwa watuhumiwa kwa pamoja walishiriki katika ufujaji wa fedha hizo zilitolewa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya nyumba za walimu na vyoo.

“Watuhumiwa hawa walikamatwa juzi majira ya saa nne usiku nyumbani kwa ofisa huyo wa Takukuru wakiwa wamempelekea kiasi hicho cha pesa ikiwa ni sehemu ya Sh. milioni nne walizokuwa wamemwahidi,” alisema.

Kiongozi huyo wa Takukuru alisema uchunguzi wa tuhuma hizo bado unaendelea na utakapokamilika, watuhumiwa wote wawili watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Mwaka 2007.

“Takukuru inatoa wito kwa wananchi kuongeza kasi ya ushirikiano kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa, pia kujitokeza mahakamani pindi wanapohitajika kutoa ushahidi wao,” aliomba.

Elinipenda pia alibainisha kuwa katika kipindi cha Januari hadi Aprili mwaka huu, Takukuru mkoani hapa imewapandisha kizimbani watuhumiwa 13 wanaokabiliwa na tuhuma mbalimbali za vitendo vya rushwa.

“Vilevile, katika kipindi husika, Takukuru mkoani hapa ilifanya operesheni maalum ya kufuatilia vyama vya ushirika, kupitia zoezi hili jumla ya fedha kiasi cha zaidi ya Sh. milioni 48.907) ziliokolewa,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live