Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ofisa TRA mbaroni rushwa ya mil 8/-

708621939593f17d2effff0a58175f49 Ofisa TRA mbaroni rushwa ya mil 8/-

Thu, 1 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza imemkamata Ofi sa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa mkoa huo, Mary Moyo (34) kwa tuhuma ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh milioni nane.

Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Daudi Nyamukama alisema jana kuwa taarifa za uwepo wa tukio hilo la kuomba rushwa ziliifikia taasisi hiyo baada ya Mary kuomba kiasi hicho cha fedha kutoka kwa mfanyabiashara mmoja wa jijini Mwanza.

Nyamukama alizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Takukuru, kwa niaba ya Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza. Alisema, Mary aliomba rushwa ili arekebishe hesabu za mfanyabiashara huyo na kuteng’eneza “Control number,” ya deni analodaiwa, kwa ahadi kuwa baada ya kupewa fedha hizo angempunguzia deni kutoka Sh 97,156,994 hadi Sh 35,000,000 .

Nyamukama alisema, Mary alikiuka Kifungu cha 15(1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007. Alisema kwa nyakati tofauti, mfanyabiashara huyo alielezwa kuwa alikuwa anadaiwa deni la kodi ambayo hakuwa na kumbukumbu nayo na baadaye alipewa TRA mkoa wa Mwanza ilimpa barua ikionesha kuwa ana deni la Sh 97,156,994.

“Hata Ofisa huyo wa TRA alimshawishi mfanyabiashara huyo alipe kiasi cha Sh 35,000,000 kwa makubaliano kwamba kati ya kiasi hicho cha fedha, Ofisa atapewa za kwake Sh 8,000,000 ili amteng’enezee deni la Sh 27,000,000 ambalo angelilipa kwa control numbe,” alisema Nyamukama.

Alisema Septemba 29 mwaka huu Mary alimpigia simu mfanyabiashara huyo kumueleza kuwa afike eneo la St Dominic Nyakahoja Mtaa wa Balewa, Kata ya Isamilo jijini Mwanza ili ampatie kiasi hicho cha fedha.

“Rushwa hupofusha waonao, baada ya mfanyabiashara huyo kufika eneo la tukio la kumkabidhi Mary fedha aliyoiomba, Mary aliipokea na kuiweka kwenye begi lake la kompyuta, na ghafla maofisa wa Takukuru walifika katika eneo hilo na kumuweka chini ya ulinzi, Mary aliangua kilio na kuomba msamaha, mara baada ya kugundua kuwa amekamatwa na Takukuru,” alisema Nyamukama.

Takukuru imempongeza mfanyabiashara huyo kwa kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa, kwa sababu alitoa taarifa iliyofanikisha kukamatwa kwa Mary

Chanzo: habarileo.co.tz