Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

OCD Kyerwa atuhumiwa kusindikiza kahawa ya magendo

21284 KAHAWA+PIC TanzaniaWeb

Mon, 8 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi awachukulie hatua askari polisi wote wa wilaya ya Kyerwa wanaotuhumiwa kusindikiza kahawa ya magendo inayouzwa nchi jirani akiwemo mkuu wa polisi wa wilaya hiyo, Justin Joseph.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Jumapili, Oktoba 7, 2018 baada ya kukagua kiwanda cha kukoboa kahawa cha Nkwenda wilayani Kyerwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Kagera.

“Askari polisi wa wilaya ya Kyerwa pamoja na OCD wao wanatuhumiwa kusindikiza kahawa inayosafirishwa kwa njia ya magendo kwenda nchi jirani kupitia njia mbalimbali zisizo rasmi zikiwemo za Kumisongo, Kashaijo na Omukatoma,” amesema Majaliwa.

Taarifa iliyotolewa kwa umma na kitengo cha mawasiliano ya ofisi ya Waziri Mkuu imemnukuu Majaliwa akisema ni jambo la hatari kama askari polisi wanasindikiza kahawa inayouzwa kwa magendo.

Amesema jambo hilo lidhibitiwe haraka, “Marufuku kupeleka kahawa nje ya nchi kwa njia ya magendo na polisi msishiriki.”

Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu amesema kuanzia msimu ujao wa kahawa, minada yote ya kahawa inayozalishwa mkoani Kagera itafanyika ndani ya mkoa huo badala ya kufanyika Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Waziri Mkuu amesema minada yote ya kahawa ikifanyika mkoani Kagera itawawezesha wakulima kulipwa fedha zao kwa muda mfupi na pia itapunguza makato  yasiyokuwa ya lazima ambayo ni kero kwa wakulima.

“Wanunuzi watafuata kahawa ilipo, utaratibu huu utawawezesha wakulima kulipwa fedha zake kwa wakati. Mnada ukifanyika katika maeneo ya uzalishaji utamuwezesha mkulima kujua bei, tofauti na unavyofanyika Moshi kwani ni rahisi mkulima kuibiwa,” amesema.

Waziri Mkuu amewataka wananchi kuendelea kuwa na imani na Serikali yao ambayo imedhamiria kuwaletea maendeleo na kwamba itahakikisha kila mmoja anapata haki yake wakiwemo wakulima ambao watasaidiwa katika kutafutiwa masoko ya mazao yao.

Chanzo: mwananchi.co.tz