Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nyumba 20 zachomwa moto Shinyanga

21308 MOTOT+PIC TanzaniaWeb

Tue, 9 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Shinyanga. Nyumba 20 za watu wanaotuhumiwa kwa matukio ya mauaji katika kijiji cha Mwenge mkoani Shinyanga zimechomwa moto na watu wasiojulikana.

Nyumba hizo zinaelezwa kuwa ni za na baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wanaodaiwa kujinasibu mitaani kwamba licha ya matukio wanayoyafanya polisi hawawezi kuwatia nguvuni kwani ni rafiki zao.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mwenge, Amos Lububu alisema tukio hilo lilitokea jana Oktoba 6, 2018 saa nne asubuhi baada ya kusikia kengele ya sungusungu imegongwa bila kujua aliyeigonga.

Mtendaji wa kijiji cha Mwenge, Paschal Chuma alisema kijiji hicho kina jumla ya watu 5,427 ambapo kumekuwa na malalamiko ya wananchi kutuhumiwa kwa mauaji na ujambazi kukamatwa na jeshi la polisi kisha muda mfupi baadaye kuachiwa huru na kuonekana mitaani wakijigamba kitendo ambacho kinaongeza hasira kwa wananchi.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga,  Alchelaus Mutalemwa akizungumza na Mwananchi leo Oktoba 7, 2018 amesema ni kweli tukio la nyumba kuchomwa moto limetokea kwa wananchi kujichukulia sheria mkononi huku akidai uchunguzi unaendelea ili kubaini waliohusika.

Amesema nyumba 20 zenye familia tano zilichomwa moto ambapo katika harakati za kuwaomba wananchi waache kuendelea kumshambulia mtuhumiwa Lole Yusuph aliyekuwa amewekwa chini ya ulinzi, mwenyekiti wa kijiji naye akajeruhiwa jichoni kwa kupigwa jambo lililowalazimu polisi  kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi hao waliokuwa na hasira kali.

“Nilisikia kengele imegongwa saa nne asubuhi nikashangaa kuna nini, nilipofuatilia nikakuta wananchi wamekusanyika na kuambiwa chanzo cha tukio ni watuhumiwa wa mauaji kuonekana mitaani wako huru na kujigamba,’’ amesema Lububu.

Amesema familia tatu zinatuhumiwa kuhusika na mauaji kwani Julai 28, mwaka huu mwanamke mmoja alinyongwa na wananchi na aliyetuhumiwa na wananchi kufanya ukatili huo ni miongoni mwa watuhumiwa ambao nyumba zao zimechomwa moto.

Baada ya polisi kufika eneo la tukio na kuwatawanya wananchi kwa mabomu na kukamata watu wanane, walipoondoka ndipo wananchi walishikwa na hasira na kwenda kuchoma nyumba za watuhumiwa.

Watuhumiwa ambao nyumba zao zimechomwa moto ni   Charles Nziku, nyumba mbili na gari moja, Loleli Yusuph,   Malenga Lubegula, Nchema  Bundala, ambapo  inaelezwa  walikamatwa  na kuwekwa ndani kwa miezi miwili  tu na kuachiwa.

Diwani  wa kata ya Mwenge  Edward Maganga amesema alipigiwa simu na mwenyekiti wa kijiji baada ya kufika kwenye  eneo la mkusanyiko wa wananchi.

Amesema alipofika ndipo alipiga simu polisi nao walifika  hapo na kuwakuta wananchi wamejawa na hasira wakaanza kurusha mawe na fimbo hadi kuvunja vioo vya gari la polisi na kulazimika kutumia mabomu ya machozi kutawanya watu.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz